Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Wizara ya Afya ya Nchi hiyo imethibitisha kuendelea kushirikiana na Mataifa rafiki ya Bara la Afrika katika mikakati yake ya kuwapatia huduma bora za Afya Wananchi wa Mataifa hayo Rafiki.

Kauli hiyo imetolewa na na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Feng Yong wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Feng Yong aliyeambatana na Ujumbe wa Madaktari na Wafanyakazi 14 wa Wizara ya Afya ya China ambao wapo Nchini kurikodi filam Maalum ya Miaka 50 ya Maendeleo ya Ushirikiano wa pamoja wa Sekta ya Afya kati ya China na Afrika amesema bado jamii ya walio wengi Barani Afrika wanaendelea kukosa huduma za Afya hasa Vijijini.

Alisema Mpango wa Nchini hiyo kutoa Madaktari Bingwa kufanya kazi za Huduma ya Afya katika Mataifa Ya afrika Ikiwemo Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla utadumishwa na kuzingatiwa zaidi.

Mkurugenzi huyo wa Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Feng Yong ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wananchi wake kutokana na ushirikiano wao kwa madaktari Mabingwa wa China wanaofanya kazi Zanzibar.

“ Tumeshuhudia ushirikiano huo wa karibu uliopo kati ya Wananchi wa Zanzibar na Madaktari wetu hali inayopelekea wengine kuamua kutaka kubakia Nchini kuendelea kutoa huduma”. Alisema Bwana Fenga Yong.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema China imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhaba wa Madaktari uliopo hapa Zanzibar.

Balozi Seif alisema inapendeza kuona Taifa la China linaendelea kuunga mkono juhudi za Zanzibar katika kuwapatia huduma za afya Wananchi wake ukiwemo mpango ulioanzishwa miaka ya Nyuma wa Nchi hiyo kutoa fursa za upendeleo kwa Madaktari bingwa wa Zanzibar kupata Taaluma zaidi ya Juu Nchini china.

“ Bahati nzuri mimi mwenyewe binafsi wakati nikiwa Balozi wa Tanzania Nchini China nimeshuhudia madaktari kadhaa wa Zanzibar niliwapokea Nchini humo walipokwenda kupata mafunzo ya Juu ya Udaktari Bingwa Nchini China”. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliomba utaratibu huo kama umesita au kupungua ni vyema ukaendelezwa zaidi ili kutoa fursa ya kuwa na watendaji wa kutosha wa sekta ya Afya kwa lengo la kuufanikisha mpango wa Zanzibar wa kuwa na Vituo cha Afya kila baada ya kilomita Tano.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imejipanga kuzingatia mpango wa kuwapatia mafunzo ya Afya Wanafunzi wanaomaliza Elimu ya vyuo vikuu na Diploma utakaokidhi mahitaji ya Sekta hiyo muhimu kwa ustawi wa Jamii Nchini.

Aliuhakikishia ujumbe huo wa Madaktari na Watendaji wa Wizara ya Afya ya Jamuhuri ya Watu wa China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukuwa jitihada zaidi za kuwapatia huduma nzuri Madaktari Mabingwa wa China wanaotoa huduma hapa Zanzibar.

Alisema Wananchi walio wengi hapa Zanzibar wameonyesha kuendelea kuridhika pamoja na kufurahia huduma mbali mbali bora za Afya zinazotolewa na Madaktari Bingwa kutoka China.

Naye Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo hapa Zanzibar Bibi Chen Qiiman ambae aliambatana na Ujumbe huo alieleza kwamba mpango maalum utaandaliwa kwa baadhi ya Madaktari wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na ile ya Abdulla Mzee Kisiwani pemba wa kuwapatia mafunzo Nchini china katika dhana ya kuzijengea uwezo zaidi wa kutoa huduma Hospitali hizo kubwa Mbili hapa Zanzibar.

Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba iko katika hatua za mwisho za kufanyiwa matengenezo makubwa ya majengo na Vifaa muhimu vya uchunguzi wa Afya pamoja na vitanda 60 vya kulaza Wagonjwa chini ya ufadhili wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top