Wananchi wa shehia tofauti zilizomo ndani ya Jimbo la Kitope wamepata fursa ya kukutana na Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi katika utaratibu aliojipanga Mbunge huyo wa kukutana nao ili kusikiliza Kero na changamoto zinazowakabili katika harakati zao za kila siku.

Mkutano wa Mbunge huyo ulifanyika katika Ofisi ya Jimbo hilo iliyopo Kijiji cha Kitope ikiwa ni miongoni mwa Ofisi kadhaa zilizojengwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo maalum la kutoa nafasi kwa wananchi kukutana na Waheshimiwa Wabunge wao.

Wananchi wasiopungua ishirini na Tatu walipata fursa hiyo ya kukutana na Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakielezea na kushauri masuala tofauti yakiwemo yale ya Jamii, Binafsi,Maendeleo na hata ya Kiuchumi.

Miongoni mwa masuala hayo muhimu yaliyowasilishwa na Wananchi hao kwa Balozi Seif ni changamoto za Vifaa vya matumizi kwa baadhi ya Majengo ya huduma za Umma pamoja na kutokamilika kwa wakati kwa baadhi ya miradi na majengo hayo.

Wawakilishi wa Kituo cha Afya cha Kitope Bibi Stara Ali na Bibi Halima Abushiri wamesema ubovu wa Uzio na ukosefu wa Tanuri la kuchomea Taka taka katika Kituo hicho imekuwa ni baadhi ya changamoto zinazowakosesha utulivu wa kutekeleza vyema majukumu yao.

Walisema upo muhumi wa kuzingatiwa kwa haraka masuala hayo kwa lengo la kuwepuka uchimbaji ovyo wa mashimo ya kuhifadhia taka ili kulinda mazingira pamoja na kuepuka kutoa mwanya kwa baadhi ya watu wenye dhamira maya ya kutaka kuhujumu Kituo hicho.

Akipata wasaa wa kufafanua pamoja na kuzitafutia mbinu baaadhi ya kero na changa moto zinazowakabili Wananchi hao wa Jimbo la Kitope Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi aliwaagiza Wananchi hao kuwa na azimio Maalum la kuhakikisha wanakamilisha Majengo yao ya Maendeleo.

Balozi Seif alisema si vyema kwa Wananchi kuendelea kuanzisha utitiri wa Miradi ya maendeleo ndani ya maeneo yao wakati uwezo wa kuikamilisha miradi hiyo kwa wakati unashindikana kutokana na ukosefu wa msukumo wa uwezeshaji.

“ Tumekuwa tukiendelea kushuhudia Miradi kibao inayoanzishwa na Wananchi wenyewe bila ya kuzingatia bajeti hali ambayo hupelekea miradi hiyo kufifia na mengine kufa kabisa kabla ya kukamilika kwake”. Alifafanua Balozi Seif.

Alisisitiza kwamba wakati umefika kwa Jamii kuhakikisha kuwa Mradi wowote unaobuniwa na hatimae kufikia maamuzi ya kuanzishwa lazima Jamii hiyo ijizatiti kwa namna yoyote ile kuhakikisha unakamilika tena kwa wakati waliojipangia.

Akizungumzia Ujenzi wa Majengo ya Umma yanayosimamiwa na Halmashauri za Wilaya Balozi Seif alilaumu baadhi ya Viongozi wa Halmashauri hizo kwa kushindwa kusimamia vyema Miradi ya Majengo hayo.

Balozi Seif alisema upo ushahidi wa majengo mengi ya Wananchi yanayosimamiwa na Halmashauri hizo ambayo hayako katika kiwango kinachostahili Kitaalamu.

Alisema usimamizi huo mbovu unaoendelea kufanya na baadhi ya Viongozi hao wa Halmashauri hizo umepelekea upotevu wa fedha nyingi za Umma na hata baadhi ya Taasisi za Wananchi katika maeneo yao.

Kuhusu Ukosefu wa Huduma ya Umeme katika Kijiji cha Mgambo Balozi Seif aliwataka Wananchi hao kuwa na subra wakati jitihada za Uongozi wa Jimbo hilo zikiendelea kwa kuwasiliana na Uongozi wa Shirika la Umeme Zanzibar katika njia ya kulitafutia Ufumbuzi Tatizo hilo la muda mrefu.

“ Moja kati ya suala gumu, ghali na linalohitaji fedha nyingi katika dunia hii ni miradi ya huduma za Umeme popote pale. Sasa kuna haja ya kushirikiana pamoja kati ya pande zote zinazohusika ili kuona namna gani tutafikia ufumbuzi wa kulitatua kero lenu hili la muda mrefu ”. Alisisitiza Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope.

Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top