Serikali ya Uholanzi inakusudia kuunga mkono harakati za Kiuchumi na Maendeleo katika Mpango wake wa kusaidia Mataifa Manane machanga Ulimwenguni.
Serikali ya Uholanzi inakusudia kuunga mkono harakati za Kiuchumi na Maendeleo katika Mpango wake wa kusaidia Mataifa Manane machanga  Ulimwenguni.
Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Dr. Ad Koek Koek alieleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Koek Koek alisema Mataifa hayo manane yaliyoko Latin Amerika pamoja na Afrika Tanzania ikiwa miongoni mwake yanatarajiwa kufaidika na Mpango utakaohusisha miradi ya pamoja kati ya Makampuni ya Uholanzi na yale ya Mataifa Washirika.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na utengenezaji wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Uwanja wa Ndege sambamba na Miundo mbinu ya Bara bara ambapo utekelezaji wake utaanza mwezi julai mwaka 2013 mara baada ya kukamilika kwa tathmini pamoja na Bajeti ya Mpango huo.
“Tumependekeza katika kusaidia kunyanyua Uchumi wa Mataifa Rafiki tumeonelea ni vyema Miradi itakayoanzishwa iwe katika mfumo wa ubia kwa lengo la kuyapa nguvu za Kiuchumi Makampuni na Taasisi za kizalendo”. Alifafanua Balozi Koek Koek.
“ Kitu kitakachozingatiwa zaidi katika mpango huo muhimu ni kuhakikisha wawekezaji wa Makampuni ya pande hizo mbili yanadumisha Ushirikiano wa karibu zaidi”. Aliendelea kusisitiza Balozi Koek Koek.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua zake iliyochukuwa ya kurejesha hali ya Amani na Utulivu iliyoterereka kufuatia vurugu za hivi karibuni zilizosababishwa na baadhi ya Vijana wa Kihuni.
Balozi Koek Koek alifahamisha kwamba hakuna Jamii inayopendelea kuona inaendelea kuishi katika mazingira yasiyokuwa na furaha kutokana na kukosekana kwa amani popote pale Duniani.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimueleza Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania kwamba Taifa pamoja na Wananchi wote wanahitaji kuona amani ya Nchi inaendelea kudumu wakati wote.
Balozi Seif alisema Amani iliyopatikana Zanzibar tokea kuanzishwa kwa mfumo wa Muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imepelekea kunyanyuka kwa Uchumi hasa katika Sekta ya Utalii kulikopelekea kuongezeka kwa Miradi ya Kitalii iliyoongeza Mapato na Ajira hasa kwa Vijana.
“ Tukiitumia vibaya bahati hii iliyomo ndani ya Sekta ya Utalii ambayo imeshaanza kutoa matumaini tutakuja kuijutia bahati hii na wala hatutakuwa na wakumlalamikia”. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif aliipongeza Uholanzi kwa mchango wake mkubwa inayoendelea kutoa kwa Tanzania na Zanzibar kwa jumla hasa katika Miradi ya Elimu, Kilimo, Afya pamoja na Miundo mbinu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi wa Uholamzi Nchini Tanzania Dr. Ad Koek Koek kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na jitihada za kuimarisha Miundo mbinu ya Bandari yake kwa lengo la kuiwezesha kutoa huduma bora katika kiwango cha Kimataifa.
Balozi Seif aliiomba Uholanzi kufikiria namna ya kusaidia ushauri na Taaluma kwa kuboresha Bandari ya Malindi kwa vile Nchi hiyo tayari imeshakuwa na uzoefu wa kutosha kutokana na uendeshaji wa Banadari yake ya Kimataifa ya Roterdam.
“ Kuimarika kwa Bandari ya Zanzibar katika kutoa huduma Kimataifa kwa kiasi Fulani kunaweza kusaidia kutoa ajira pamoja na kukuza Uchumi ambao hivi sasa unategemea zao la karafuu na Sekta ya Utalii”. Alieleza Balozi Balozi Seif Ali Iddi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top