Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amefanya ziara fupi ya kuangalia athari iliyotokea katika baadhi ya Majengo yaliyochomwa moto na kuharibiwa na Vijana wanatuhumiwa kuwa wafuasi wa Kiongozi mmoja wa Kidini hapa Zanzibar.
Matukio hayo yalioanzia mchana wa jumatano yamesabisha pia kuharibiwa kwa baadhi ya Miundo mbinu ya Bara bara kwa kuchoma moto matairi ya gari pamoja na kupangwa kwa mawe makubwa yaliyopelekea kuleta usumbufu kwa wasafiri na waendeshao vyombo vya moto.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikagua kituo kidogo cha Polisi Mkunazini ambapo Mkuu wa Kituo hicho Inpector Suleiman Mohd alimueleza Balozi Seif kwamba Vijana hao wa kihuni walitaka kuvamia Kituo hicho majira ya saa nane za Mchana wa Jumatano kwa nia ya kutaka kuhujumu Kituo hicho.
Inspector Suleiman alifahamisha kwamba kwa ushirikiano mkubwa na wa karibu kati ya Polisi na Wananchi wa maeneo ya karibu na Kituo hicho waliweza kusaidia kunusuru uvamizi huo.
Hata hivyo Kamanda Suleiman alieleza kwamba Vijana hao wa Kihuni wamefanikiwa kuichoma moto vespa moja ya Mmoja wa Askari wa Jeshi hilo la Polisi iliyokuwa imeegeshwa mbele ya Kituo hicho.
Balozi Seif pia aliangalia uharibifu uliofanywa katika Jengo la Maskani Kaka ya CCM ya Kisonge iliyoharibiwa vibaya baada ya kushambuliwa kwa Mabomu na Vijana hao wa Kihuni na kusababisha hasara kubwa ambayo hadi sasa tathmini halisi haijajuilkana.
Mmoja wa Kiongozi wa Maskani hiyo ya Kisonge Ndugu Mzee Haji Jecha alisema wanachama hao wamekuwa njia panda kuona Viongozi wa juu wa Serikali wanaendelea kuhubiri amani lakini bado hali inatisha kutokana na Vitendo viovu vinavyoashiria kuvunjika kwa amani iliyopo.
Nd. Mzee alisema Wanachama wa Maskani hiyo bado hawaoni uhalali wa Vitendo vinavyofanywa na Vijana hao kuhusishwa na uharibifu wa Majengo yao ambayo yamejengwa kwa gharama kutokana na jasho lao kwa faida ya mapumziko pamoja na kuweka vitega uchumi vitakavyosaidia kukidhi mahitaji yao ya Kimaisha.
Hata hivyo Ndugu Mzee alimfahamisha Balozi Seif kwamba Viongozi na Wanachama wa Maskani hiyo Kaka ya Kisonge hawana nia ya kulipiza kisasi kutokana na vitendo wanavyoendelea kufanyia na badala yake kuviachia vyombo vya Sheria kufanya uchunguzi na kuchukuwa hatua zinazostahili dhidi ya waovu hao.
Wanachama hao wa Kisonge wameiomba Serikali pamoja na wafadhili kungalia namna wanavyoweza kuthathmini tukio hilo na jinsi watakavyoweza kusaidia kuirejesha hali hiyo kwa vile baadhi ya Wanachama wa Maskani hiyo wameathirika vibaya baada ya biashara zao pamoja na Vipando kama Vespa kuteketezwa kwa moto kutokana na uvamizi wa Vijana hao.
Akiwapa pole waathirika wa matukio hayo pamoja na kusikitishwa na vitendo hivyo vya kihuni vilivyofanywa na Vijana hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali isingelipenda kuona Zanzibar inarejea katika maisha ya mtafaruk.
Balozi Seif alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kulitafakari tukio hili la kusikitisha linaloitia aibu Nchi mbele ya Jumuiya za Kimataifa na kujaribu kuangalia hatua zinazofaa ili kudhibiti vitendo hivyo.
Uharibifu huo uliofanywa na baadhi ya Vijana umepelekea kuharibu Majengo ya CCM ya Maskani ya Kisonge, Maskani ya Muembe ladu, Tawi la CCM Kilimahewa,miuno mbinu ya Bara bara pamoja na baadhi ya vyombo vya moto vya Wananchi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment