Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema pamoja
na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za uimarishaji wa Sekta ya
Afya lakini bado Wananchi wana wajibu wa kuchangia baadhi ya huduma katika
Sekta hiyo muhimu kwa Jamii.
Balozi Seif lisema hayo wakati akiendelea na awamu ya
pili ya Ziara yake katika Taasisi zilizomo ndani ya Wizara ya Afya Zanzibar ikiwa
ni mwanzo wa mpango wake wa kuzitembelea Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Seif ambaye alipata fursa ya kuzitembelea
Hospitali za Jimbo la Kwamtipura iliyopo Mikunguni, Kituo cha Afya cha Fuoni ,
Kituo cha Afya cha Jambiani pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Kusini iliyopo
Makunduchi alisema nia ya Serikali ni kusambaza Huduma za Afya katika maeneo
yote ya Jamii Mjini na Vijijini bila ya Malipo.
Hata hivyo alisema katika kuunga mkono juhudi hizo
Wananchi wana paswa kuchangia baadhi ya huduma katika Vituo na hospitali za
Serikali hasa pale inapohitajika kufanya hivyo kwa lengo la kuimarisha
upatikanaji wa huduma hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameuomba Uongozi wa Wizara ya Afya
Zanzibar kuangalia uwezekano wa kuitumia Hospitali ya Kwamtipura kama Tawi la Hospitali
Kuu ya Mnazi Mmoja katika baadhi ya Vitengo vyake.
Balozi Seif alisema Hospitali hiyo ingawa imejengwa
kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wakaazi wa Jimbo la Kwamtipura na maeneo ya
jirani lakini bado inaonekana kuwa na
nafasi kubwa nay a kutosha ya kutumiwa ikiwemo pia kulazwa wagonjwa.
“ Nimefurahi kuona huduma nzuri zinazotolewa na
Hospitali hii. Lakini pia zipo fursa nyingi ambazo hazijatumiwa ndani ya Hospitali
hii. Kwa nini Uongozi wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja wasiitumie fursa hizi
zilizopo?”. Alishauri Balozi Seif.
Amewapongeza Madaktari, Wauguzi na Wafanyakazi wote wa Hospitali na Vituo vya Afya vya
Kwamtipura, Fuoni, Jambiani na
Makunduchi kwa jitihada zao za kuwapatia huduma bora Wananchi.
Balozi Seif aliwahakikishai watendaji hao wa Sekta ya
Afya kwamba Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya watasaidiana katika
kuzipatia ufumbuzi changamoto na kero zinazowakabili watendaji hao katika
sehemu zao za kazi.
“ Serikali itajitahidi kuona utendaji wenu unaimarika
vyema lakini hilo
ni vyema likaenda sambamba pia na nyinyi kujitahidi kufanya kazi zaidi”.
Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akizungumzia suala la Uzio kwa Hospitali ya Wilaya
kusini huko Makunduchi Balozi Seif aliushauri Uongozi wa Hospitali hiyo
kutafuta mbinu za kuzunguusha uzio hata kama
utakuwa wa muda.
Alisema hatua hiyo itaweza kusaidia ulinzi wa eneo hilo vyenginevyo tatizo la uvamizi katika eneo hilo litashindwa
kuzuilika.
Kwa upande wao baadhi ya waratibu na wakuu wa Vituo
hivyo vya Afya walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba lipo
tatizo la uhaba wa wafanyakazi wa kudumu kwa baadhi ya vituo na Hospitali hizo
jambo ambalo linapunguza kasi ya uwajibikaji wao.
Walitoa mfano wa Mfanyakazi wa baadhi ya Vitengo kama
Meno kufanya kazi katika vituo viwili vya Afya hali inayopelekea kituo kimoja
kwa siku hiyo kukosa huduma hizo muhimu.
Hata hivyo Wakuu hao wa Vituo vya Afya na Hospitali
walifahamisha kwamba yapo mafanikio makubwa ya uimarikaji wa huduma za afya za
Wananchi kutokana na elimu kubwa inayoendelea kutolewa katika vituo hivyo hasa
suala la ushauri nasaha na Uzazi wa Mpango na salama.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dr. Saleh
Mohammed Jidawi alisema uimarishaji wa huduma za afya ya msingi katika maeneo
ya Wananchi ndio unaopelekea kupata Jamii yenye afya na nguvu za uhakika.
Dr. Jidawi alisema Zanzibar
imefanikiwa kuwa na miundo mbinu mizuri ya huduma za Afya inayotokana na kuwa
na Vituo vingi vya Afya vinavyokadiriwa kufikia 140 Unguja na Pemba.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment