Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimshukuru Naibu Mkurugenzi ambaye pia ni Mratibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } Kanda ya Dar es salaam Bwana Victor Nkya wakati Mamlaka hiyo ikiwasilisha mchango wao wa Maafa kufuatia ajali ya Meli ya M.V.Skagit Miezi miwili iliyopita.
Imeelezwa kwamba mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya matumizi mabaya ya simu iwe ya mkononi, majumbani na hata Maofisini ikiwemo matusi adhabu yake ni miezi sita Jela au Faini ya Shilingi milioni Tano au adhabu zote mbili. 
Naibu Mkurugenzi ambae pia ni mratibu wa Ofisi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } Kanda ya Dar es salaam Bwana Victor Nkya  alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Nkya aliyeuongoza Ujumbe wa Viongozi wanne wa Mamlaka hiyo na kukabidhi mchango wa Shilingi Milioni 5,000,000/- kwa Mfuko wa Maafa Zanzibar kufuatia ajali ya M.V.Skagit miezi miwili iliyopita alisema sheria na kanuni zinazohusiana na matumizi ya Simu zipo.
Alisema licha ya asilimia 95% ya sim Card zote zinazotumika Nchini Tanzania kusajiliwa katika kampuni tofauti yanayoendesha biashara ya simu lakini bado zipo hitilafu zinazopelekea baadhi ya watu kutumia vibaya fursa za matumizi hayo ya simu.
“ Mtu atakayetumia Simu kinyume na taratibu zilizoainishwa katika sheria na kanuni zilizopo endapo atapatikana na hatia adhabu yake ni jela miezi sita au faini ya shilingi Milioni 5,000,000/-”. Alisisitiza Bwana Nkya.
Naibu Mkurugenzi huyo wa Malaka ya Mawasiliano Tanzania Kanda ya Dar es salaam alifahamisha kwamba Uongozi wao upo hapa Visiwani kuangalia mazingira ya namna ya Kufungua Ofisi yao Zanzibar.
Alisema Mamlaka yao ambayo inahusiana na masuala ya Taasisi za Simu, Tv, Redio pamoja na Internet ina nia pia ya kuwa na kituo cha mtandao wa pamoja wa Internet Nchini kwa lengo la kurahisisha mawasiliano hayo.
Bwana Nkya alifahamisha kwamba hatua hiyo itakwenda samba mba na uimarishaji wa mawasiliano ya Mtandao wa Internet katika vyuo Vikuu Nchini ambao utasaidia kumuwezesha mwanafunzi wa chuo Kikuu kujisomea kwa kina  zaidi kupitia mitandao hiyo.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushukuru Uongozi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } kwa mchango wake huo uliokuja kufuatia maafa hayo ya kuzama kwa Meli ya M.V.Skagit ambayo yataendelea kukumbukwa miaka kadhaa ijayo.
Balozi Seif alieleza kwamba kitendo chao hicho ni ishara ya muendelezo  wa Mila, Silka na Utamaduni wa Waafrika katika kufarijiana wakati wana jamii wenzao wanapopatwa na misiba.
Wakati huo huo Kikao cha Taifa cha Sensa Zanzibar kimekutana mara baada ya kumalizika kwa zoezi la uandikishaji wa sensa ya watu na Makazi lililomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kikao hicho kilichoshirikisha Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Maafisa Tawala wao wa Mikoa na wilaya zote za Zanzibar kilifanyika chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Wajumbe wa kikao hicho wamekutana katika ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi uliopo Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Akitoa tathmini ya zoezi hilo la Sensa ya watu na makazi Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Nd. Mohd Hafidh alisema asilimia 87.3 ya Kaya zote za Zanzibar zimehesabiwa baada ya wiki ya nyongeza ambapo awali ilikuwa Asilimia 82.4.
Ndugu Mohd Hafidh alivipongeza vikundi vya Polisi Jamii katika shehia mbali mbali Nchini kwa kujudi zao zilizopeleka kudumu kwa usalama katika kipindi cha zoezi hilo  licha ya kuwa na matukio ya wasi wasi kwa baadhi ya shehia hizo.
Hata hivyo Ndugu Hafidh alisema zipo changamoto zilizojitokeza katika zoezi hilo ambapo miongoni mwake zikiwa ni  pamoja na baadhi ya watu kususia zoezi hilo kwa visingizio vya migogoro ya Kijamii katika maeneo yao pamoja na  suala la upatikanaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top