Uongozi wa Jimbo la Kitope umekusudia kuimarisha sekta
ya michezo kwa lengo la kuwawezesha Vijana wa Jimbo hilo kuwa pamoja katika harakati zao za
Michezo na zile za kijamii.
Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo
mara baada ya kupokea matatizo na ushauri wa wanamichezo wa Timu Nne zilizomo
ndani ya Jimbo hilo walioutoa katika Kikao chao kilichofanyika katika Ukumbi wa
Mikutano wa Ofisi ya Tawi la CCM Kitope A.
Balozi Seif aliwaeleza wawakilishi wa Timu hizo ambazo
ni Kitope United, African Boys, Home Boys na Kombora kwamba uamuzi wao wa kufikiria kuanzisha Timu moja
imara ndani ya jimbo hilo umetoa faraja
kwa viongozi jambo ambalo litarahisisha hata upatikanaji wa vifaa na misaada
kw wepesi zaidi.
Aliahidi kwa kuwa yeye ni Kiongozi wao wa Jimbo
atahakikisha kwamba Sekta ya Michezo
inapata nguvu zaidi kutokana na umuhimu wake
uliojichomoza hivi karibuni wa kutoa ajira endapo Vijana hao watajituma
vilivyo.
“ Nataka kuona Timu za Jimbo langu la Kitope
zinashiriki na kufanya vizuri katika
mashindano ya Wilaya, Mikoa na hata Taifa. Lakini kitachosaidia zaidi kwenu ni
juhudi ya kuzingatia mazoezi yatakayofuatiwa na nguvu za misaada ya Viongozi
wenu”. Alisisitiza Balozi Seif.
Akizungumzia matatizoyanayozikabili Timu hizo Balozi
Seif atajaribu kuzungumza na wafadhili
mbali mbali wa michezo ili kuona namna gani wanaweza kusaidia uimarishaji wa
uwanja wa uhakika na wa kisasa ndani ya jimbo hilo.
Alisema suala hilo litakwenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya michezo ikiwemo
Mipira, Nyavu Magoli na Jezi ambazo alisema zimo ndani ya uwezo wake kulingana
na utaratibu aliokwishauanzisha tokea alipoanza kuliongoza jimbo hilo.
Kuhusu suala la uanzishwaji wa jengo la kudumu la
Klabu Balozi Seif aliwaagiza wanamichezo hao kuanza shughuli za maandalizi ya
msingi kwa vile tayari wameshaanza kukusanya nguvu za pamoja.
Alisema katika kuunga mkono jitihada hizo za
wanamichezo atahakikisha anasaidia nguvu za unyanyuaji jengo kwa hatua ya
matofali na kuangalia mbinu za kuendeleza ujenzi huo.
Balozi Seif Ali Iddi akiwa pia Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar
aliwakumbusha wanamichezo hao kuwa
waangalifu kutokana na ushawishi wanaoendelea kusambaziwa wa kutaka kuingizwa katika vurugu za kisiasa
kwa kisingizio cha Kidini.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba ushawishi huo
unaweza kuyayusha kabisa amani na muda wa Vijana hao wa kushiriki kikamilifu
katika michezo yao
endapo wataamua kuupokea.
Mapema wanamichezo hao walimueleza Balozi Seif matatizo yanayowakabili katika katika
harakati zao za kuendeleza michezo ambayo yamekuwa yakipunguza kasi yao ya ufanisi.
Wawakilishi wa wanamichezo hao Khamis Mswahili Mwinyi,
Ngamia Mohd Ngamia na Amour Amour kwa pamoja walielezea changamoto
zinazowakabili katika sekta ya michezo ikiwa ni pamoja na uhaba wa vifaa vya
michezo, ujenzi wa Jengo la Klabu pamoja na uanzishwaji wa mashindano ya kombe
la Mbunge wa Jimbo hilo ambayo tayari yamesharidhiwa na Mbunge mwenyewe kwa
kukubali kutoa Vikombe na zawadi kwa washindi.
Walisema kufanikiwa kwa changamoto hizo kutawawezesha
Vijana waliowengi wa jimbo hilo
kuwepuka kusambaratika pamoja na vishawishi vinavyoweza kuwapelekea kujiingiza katika matendo maovu.
Katika kikao hicho Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope
Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi seti ya Jezi na Fedha Taslimu kwa Timu ya Soka
ya Kitope United inayojiandaa na usajili
kwa ajili yua mashindano yajayo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment