Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China
kwa misaada yake mikubwa inayotoa katika kuunga mkono harakati za Kiuchumi na Maendeleo
za Zanzibar.
Shukrani hizo zimetolewa na Makamu wa pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika sherehe za uzinduzi wa Ujenzi wa Skuli
mpya ya Msingi ya Mwanakwerekwe C kwa ufadhili wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu
wa China.
Uzinduzi huo umekwenda samba mba na Ubalozi wa China kukabidhi Madeski 480 ahadi ya Serikali ya
Jimbo la Sichuan Nchini China wa Yuan Milioni Moja kuipatia Zanzibar kufuatia ziara ya
Balozi Seif Jimboni humo Mwezi Oktoba mwaka 2011.
Balozi Seif alisema Madeski hayo yatasaidia kupunguza uhaba wa Vikalio kwa Wanafunzi
wa Skuli mbali mbali hasa zile za msingi za Unguja na Pemba.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mipango yake ya Maendeleo
suala la Elimu limepewa nafasi ya pekee lengo likiwa ni kuona watoto wote
wanapata fursa ya Elimu katika mazingira bora.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alimpongeza Balozi Mdogo wa China
aliyepo Zanzibar Bibi Sheen Limun kwa juhudi zake za kuunganisha uhusiano mzuri
uliopo kati ya Nchi yake na Zanzibar.
Alisema Balozi Sheen tokea amefika Nchini kuanza
kutekeleza majukumu yake amekuwa chachu ya Maendeleo ya Zanzibar hasa katika Sekta ya Elimu.
Balozi Seif amewahimiza Wanafunzi kuongeza bidii
katika masomo yao
ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali kupitia
washirika wa maaendeleo katika kuimarisha sekta hiyo muhimu kwa Taifa.
Aliwataka Wanafunzi hasa wale wa Kiume kuacha mzaha
katika kutafuta elimu vyenginevyo watakuja jikuta wakiongozwa na akina mama
katika nyadhifa mbali mbali za utumishi wa umma.
“Bila ya elimu hakuna maendeleo yoyote yale. Taifa
kukosa wataalamu mara zote zinakuwa butu. Tunashukuru sana
kwamba Zanzibar
haiko huko. Lakini hata hivyo vijana hasa wa kiume mnapaswa kuacha mzaha katika
kusaka Elimu”. Alisisitiza Balozi Seif.
Akitoa nasaha zake Balozi mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa
China Bibi Sheen Limun
alisema China wakati wote
itazidi kuongeza nguvu zake kwa Zanzibar
katika kujenga mazingira bora ya Kielimu.
Bibi Sheen aliwahakikishia wanafunzi wa Zanzibar kwamba jitihada
zinazochukuliwa na Serikali kupitia marafiki zitasaidia kuwajengea mazingira
mazuri ya elimu wanafunzi hao.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mfunzo ya
Amali Bibi Mwanaidi Saleh alisema Ujenzi wa
Skuli hiyo mpya ya Mwanakwerekwe C ulioanza mwezi huu unatarajiwa
kukamilika Mwezi Marchi mwaka ujao wa 2013.
Bibi Mwanaidi alifahamisha kwamba Jengo hilo litakalogharimu
jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 1.6 litakuwa na Madarasa 12, Ofisi ya
Mwalimu Mkuu, Maktaba na Chumba cha Kompyuta.
Ujenzi huo unaogharamiwa na Serikali ya Jamuhuri ya
Watu wa China
ni wa pili ukitanguliwa na ule wa Skuli ya Msingi ya Kijichi iliyoko Wilaya ya
Magharibi.
Jumla ya Skuli 13 za Msingi Unguja na Pemba
zimefanikiwa kugaiwa madeski hayo 480 kutoka msaada wa Serikali ya Jimbo la Sichuan Nchini China.
Skuli hizo ni pamoja na Bububu, Ukongoroni, Makadara,
Karume Donge,Kitope, Kijichi, Matetema, Charawe, Donge Mtambile, Muembe Shauri,
Rahaleo, Karange na Kidagoni.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment