Serikali zote mbili ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeziagiza Mamlaka zinazosimamia usafiri wa Baharini za Sumatra ya Tanzania Bara na ZMA ya Zanzibar kufanya kazi kwa mashirikiano zaidi ili kupata ufanisi na kuondoa kasoro zinazoweza kuleta hitilafu ya kiutendaji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Timu ya Wabunge wa Bunge la Muungano hapo ukumbi wa juu wa Baraza la Wawakilishi Mbweni ambao walifika Zanzibar kutoa mkono wa pole kufuatia ajali ya Meli ya M.V Skagit iliyotokea kati kati ya wiki hii.
Balozi Seif aliueleza Ujumbe wa Wabunge hao walioongozwa na Spika wake Mh. Anna Makinda kwamba mashirikiano hayo yanaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuwepuka hitilafu za vyombo wakati vinapotoa huduma ya usafiri kwa abiria wa pande zote mbili.
“ Baadhi ya Wafanyabiashara wetu wamekuwa na tabia ya kutuletea vyombo kachara vilivyochakaa kutoa huduma ipasavyo ambavyo ni hatari kabisa kuvitumia kwa maisha ya wasafiri wetu”. Alieleza Balozi Seif Ali Iddi.
Alisema Serikali hizo zimesisitiza kwamba kazi za mashirikiano hayo kwa mamlaka hizo ni vyema zilenge zaidi katika shughuli za upasishaji wa vyombo husika.
“ Itapendeza na kujenga mazingira bora inapotokezea mamlaka moja ikitoa maamuzi kuhusiana na chombo chenye hitilafu ya kiufundi na ile ya Pili kuweka baraka zake. Hii inatokana na sababu ya vyombo hivyo vya usafiri kuhudumia Wananchi wa pande zote mbili”.Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alieleza kwamba Serikali itajitahidi kwa kufanya uchunguzi wa kina na kitaalamu kuona iwapo vyombo vya usafiri vilivyopo hivi sasa vinafaa kuendelea kutoa huduma.
Akizungumzia suala la janga la Meli ya M.V Skagit Balozi Seif aliueleza Ujumbe wa Wabunge hao wa Bunge la Muungano kwamba Wazamiaji wa Israel walioko katika Hoteli ya Kitalii Nungwi kwa kushirikiana na Timu ya wazamiaji wazalendo wanaendelea na zoezi la kuitafuta Meli hiyo ya M.V Skagit.
Alisema zoezi hilo la uchunguzi wa kuitafuta Meli hiyo lilianza jana katika eneo ilipozamia la karibu na Kisiwa cha Chumbe bila ya mafanikio licha ya kina kidogo cha maji cha Mita 30 hadi 38 ikilinganisha na kile cha Mkondo wa Nungwi.
Alisema siku tatu za maombolezo zimemalizika hivyo amewakumbusha waumini wa Dini na madhehebu mbali mbali pamoja na Wananchi kuwaombea dua katika majengo yao ya Ibada hapo kesho wale  marehemu waliotangulia mbele ya haki kutokana na ajali hiyo. Balozi Seif alifafanua kwamba Serikali imeshatoa ruhusa kwa Wananchi watapozipata maiti za wahanga wa ajali hiyo kuizika sehemu hiyo hiyo kulingana na muda ulivyopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Ujumbe huo wa Wabunge ukiongozwa na Spika Makinda kwa kitendo chao cha kuja kufariji wafiwa ambacho kinathibitisha kuguswa kwao na tukio hilo.
Akitoa shukrani kwa Niaba ya Timu ya ujumbe wa Wabunge hao Mbunge wa Jimbo la Magomeni Mh. Mohd Amour Chombo amezipongeza jitihada za Serikali zote mbili zilizochukuliwa katika kukabiliana na janga hilo.
Mh. Chombo alisema hatua hiyo ya muda mfupi imesaidia kunusuru vifo na majeruhi kadhaa wa ajali ya Meli hiyo ya M.V Skagit. Hadi jana jioni wazamiaji kwa kushirikiana na Vikosi vya Ulinzi vya pande zote mbili Nchini wameweza kuokoa jumla ya Maiti 68 na waliohai ambao wengine walipata majaraha 146.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top