Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kujenga misingi imara ya kukuza ubia baina ya Sekta ya Umma na ile Binafsi ili kuwajengea uwezo Wazanzibari kushiriki kikamilifu katika shughuli za Kiuchumi Nchini. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed ameeleza hayo wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  kwa Mwaka wa fedha wa 2012/2013 katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea kwenye ukumbi wa Baraza hilo hapo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mh. Aboud alisema misingi hiyo { Public –Private Partnership } itakwenda sambamba na Sekta Binafsi kuwekeza kwenye Miradi mbali mbali ya Maendeleo ya Kiuchumi na Utoaji wa Huduma. Waziri Aboud alifahamisha kwamba Sekta Binafsi ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa Uchumi wa Taifa, hivyo kupitia  uwekezaji wa Sekta hiyo Nchi itakuwa na fursa kubwa  ya kuongeza  Pato la Taifa pamoja na ajira kwa Vijana. 
Mh. Aboud alieleza kwamba  katika kuweka mazingira mazuri  ya kukuza fursa za uwekezaji, Serikali kwa kushirikiana na Wahisani tofauti itaimarisha  zaidi miundo mbinu ili kutanua wigo wa  eneo hilo muhimu. Aliitaja miundo mbinu hiyo kuwa ni pamoja na Umeme, Bara bara, Bandari ikiwemo ujenzi wa njia ya pili ya Umeme kutoka Ubungo Dar es salaam hadi Mtoni Unguja. 
Akizungumzia suala la Migogoro ya Ardhi iliyoibuka zaidi katika miaka ya hivi karibuni Waziri Aboud alisema Ofisi hiyo  tayari imeshapokea malalamiko 35 yanayohusu migogoro ya Ardhi kutoka kwa Watu na Taasisi tofauti Nchini. 
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kwamba Viongozi na baadhi ya Watendaji  katika Wizara husika , Mikoa, Wilaya, Masheha na hata Wananchi ni sehemu ya tatizo hilo kubwa linaloonekana kutofuatwa kwa taratibu na sheria za umiliki na uhaulishaji wa Ardhi. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionya kwamba Serikali haitawavumilia Viongozi na watendaji wanaojihusisha na Migogoro ya Ardhi  na hatua za kisheria zitachukuliwa  dhidi yao ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi. 
Alikumbusha kwamba maagizo ya Serikali ni kuwataka Wakuu wa Mikoa,Wilaya pamoja na Wiazara inayoshughulikia  masuala ya ardhi kuendelea  kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo ili kurejesha  imani ya Wananchi kwa Serikali yao. 
Alisema ni vyema utaratibu huo ukaenda sambamba na  kutolewa Elimu kwa Wananchi juu ya umuhimu wa kufuata sheria na taratibu za matumizi bora ya ardhi kwa lengo la kuwepuka migogoro. 
Kuhusu suala ya mchakato wa Katiba Mpya ya Muungano, Waziri Aboud alisema hiyo ni moja ya hatua muhimu itakayokidhi matakwa ya Wananchi na kuhakikisha maslahi ya kila upande  wa Muungano yanalindwa ipasavyo. 
Waziri Aboud amewaomba Wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa Maoni yao kwa Uhuru na bila ya woga wakati utakapowadia. 
Aliwasihi Viongozi kuwaelimisha Wananchi juu ya utaratibu wa kutoa maoni kwa kuzingatia sheria Nambari 8 ya mwaka 2011 kama ilivyorekebishwa  na sheria nambari 2 ya mwaka 2012 ya mabadiliko ya Katiba. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba hiyo ni fursa adhimu kwa wananchi wote wa Tanzania tokea  kuasisiwa kwa Taifa hili, hivyo ni vyema wananchi wakaitumia vyema fursa hiyo kwa faida ya Taifa zima. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed ameliomba Baraza la wawakilishi kuidhinisha  Jumla ya shilingi Bilioni 22,366,010,000/- kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Taasisi zake kwa matumizi ya Kawaida na Maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013. 
Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top