Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni mbunge wa Jimbo la kitope Balozi Seif Ali Iddi amevutiwa na moyo na kauli ya wanamichezo wa Timu ya Soka ya Mkoa wa Kaskazini Unguja ya kwenda kushinda katika mashindano ya Copa Coca Cola yanayoanza Mwishoni mwa Wiki hii Mjini Dar es salaam.
Balozi Seif ametoa Kauli hiyo mapema asubuhi wakati alipoitembelea Kambi ya Vijana 20 na Viongozi 7 wa Timu hiyo na kuifunga rasmi hapo katika jengo la Kituo cha Huduma Rafiki Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema yeye pamoja na Viongozi wenzake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja watajitahidi kuhakikisha ushiriki wao kwenye mashindano hayo hautakuwa na Matatizo.
“ Nitahakikisha ombi lenu la kutembelewa na Waheshimiwa Wabunge na Wawakilishi kwenye mashindano yenu nitalifikisha sambamba na kuwataka waje na wachangie huduma zenu huko mliko”. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwakumbusha kwamba cha kuzingatia zaidi ni Ushirikiano baina yao na wenzao kwenye mashindano hayo kwa vile Michezo mbali ya Mashindano lakini mara nyingi hujenga na kuleta Urafiki.
Balozi Seif katika kujenga Mazingira mazuri ya ushindi kwa Wanamichezo hao amekabidhi Mchango wa Shilingi Laki Saba Taslim { 700,000/- } kwa ajili ya ununuzi wa Viatu ili wafikie daraja la kucheza katika mfumo wa Kisasa wa Mchezo huo.
Aliwaomba safari yao ya Mashindano iwe ya kushinda na sio kushiriki kwa vile mara zote kwenye michezo ipo sifa ya kushinda na si vyenginevyo.
“ Kitu muhimu ni kucheza kama Timu moja, mchezaji asitake kuonyesha ufundi wa kupiga chenga kupita kiasi kwani hatakuwa na uwezo wa kushinda peke yake”. Alilisisitiza hilo Balozi Seif.
Balozi Seif alisema hitilafu ndogo ndogo katika michezo haiepukiki lakini kinachowapasa Vijana hao kuzingatia zaidi nidhamu na kuwepuka hasira wakati wawapo Viwanjani.
Ameahidi kuwatembelea watakapokuwa Mashindanoni iwapo wakati utamruhusu endapo atapata wasaa wa kupita Mjini Dar es salaam katika majukumu yake ya kikazi.
Balozi Seif alieleza zaidi kwamba utaratibu unaendelea kufanywa wa kuwapatia Tiketi za usafiri wa Dar es salaam Wanamichezo hao na kuahidi kuwagharamia Viongozi Wawili ambao hawamo katika ule utaratibu wa Idadi ya Viongozi watano wanaopaswa kuambatana na Timu husika katika Mashindano hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Viongozi wa Serikali na ZFA wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa juhudi zao za kukaa nao pamoja Wanamichezo hao kwenye Kambi hiyo.
Alisema Kitendo hicho cha kuwanoa Vijana hao kinaashiria mategemeo makubwa ya Wawakilishi hao wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kufanya vizuri katika mashindano hao.
Katika Risala yao iliyosomwa na Mshika Fedha wa ZFA Wilaya ya Kaskazini “B” Mosi Ame Mosi Wanamichezo hao walimpongeza Balozi Seif kwa moyo wake wa kijasiri uliopelekea kuwajengea hamasa ya kurejea Mkoani humo na matumaini makubwa ya kufanya vizuri.
Mosi Ame Mosi alimueleza Balozi Seif kwamba Vijana hao wa umri wa chini ya Miaka 17 wamewiva na wako tayari kimashindano licha ya matatizo madogo madogo ambayo si kikwazo katika malengo yao ya ushindi.
Mashindano hayo ya Copa Coca Cola yaliyoandaliwa na Kampuni ya Coca Cola Tanzania yanatarajiwa kuanza Tarehe 23 June 2012 katika Viwanja vya Karume, Kawe pamoja na Tamco na kumalizika Tarehe 6 Julai 2012 yakijumuisha takriban Makundi manne.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top