Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kupokea msaada wa Vikalio kwa ajili ya Wanafunzi wa Skuli za Zanzibar ndani ya kipindi cha Miezi sita ijayo. Msaada huo unaogharimu jumla ya shilingi milioni mia tatu na ishirini {320,000,000/- } umetolewa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Kampuni ya Nain Jin Tax ya Jimboni Sichuan.
Balozi Mdogo wa China Hapa Zanzibar Bibi Sheen Limun alieleza hayo wakati akizuungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Bibi Sheen alisema Msaada huo umekuja kufuatia Ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyoifanya katika Jimbo la Sichuan Nchini China ambapo Kampuni hiyo iliahidi kutoa msaada huo mwezi Oktoba mwaka jana.
Katika Ziara hiyo Balozi Seif alimuakilisha Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda kwenye Tamasha la 12 la Maonyesho ya Biashara Jimboni Sichuan yaitwayo { Western China Expo }.
Balozi Sheen alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Msaada huo umeelekezwa kwenye Vikalio kuzingatia Skuli nyingi za Zanzibar zinakabiliwa na uhaba wa Vikalio.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa jitihada zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar. Balozi Seif alisema msaada huo kwa kiasi kikubwa utasaidia kupunguza tatizo la vikalio kwa wanafunzi walio wengi hapa Nchini.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Utalii katika Jimbo la Calirfonia Nchini Marekani Bwana Richard Soyomba.
Katika mazungumzo yao Bwana Soyomba ambaye amekuja Nchini kufuatia ziara ya Balozi Seif aliyoifanya nchini Marekani mwishoni mwa mwaka jana ameelezea kufurahishwa kwake na hali ya mazingira iliyopo hapa Zanzibar.
Bwana Soyomba ameahidi kwamba Taasisi yake itajaribu kuyashawishi Makampuni mbali mbali Nchini Marekani kuja kuwekeza hapa Zanzibar katika Sekta za Nyumba, Utalii na Umeme. Alitoa mfano wa Mradi za umeme unaotumia Jua ni muwafaka kwa mazingira ya Zanzibar kwa vile unaweza kuendeshwa na Wahandisi wazalendo wenyewe baada ya kupatiwa mafunzo. Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimueleza Bwana Soyomba kwamba Serikali itakuwa tayari kushirikiana na Makampuni au Taasisi zozote zilizoamuwa kuekeza Nchini kwa lengo la kustawisha Maisha ya Jamii.
Alisema Mipango maalum itaandaliwa na Taasisi husika zinazosimamia miradi tofauti Nchini ili kuona Makampuni ya Marekani yanaweza kuwekeza miradi yao Nchini.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Mtandao wa Kibiashara { Global Trade 2020 Limited } Bibi Yichen Mao alisema Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa zaidi ya Maendeleo endapo itakuwa na Miundo mbinu makini ya Umeme.
Bibi Yichen na Ujumbe wake alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuhusiana na Mradi wa Umeme wa jua unaosimamia na kuendeshwa na Taasisi hiyo katika sehemu tofauti Duniani.
Alisema Taasisi yake imelenga kuelekeza nguvu zake za uzalishaji wa kiwango kikubwa cha umeme katika ukanda wa Mashariki mwa Bara la Afrika.
Akiushukuru Uongozi wa Taasisi hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushauri Uongozi huo kukaa pamoja na Watendaji wa Taasisi husika Nchini ili kuona jinsi gani wanaweza kupata mwanga wa kuujadili vyema mradi huo muhimu.
Balozi Seif alisema Zanzibar hivi sasa ina kianzio kimoja tu cha umeme jambo ambalo huleta usumbufu wakati inapotokezea hitilafu ya kiufundi. Taasisi ya Kimataifa ya Mtandao wa Kibiashara tayari imeshawekeza miradi ya umeme inayotumia nguvu ya jua katika Mataifa ya Spain, Italy, Bulgari kwa ulaya na Angola na Ghana kwa Afrika.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top