Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameombwa Kushirikiana na Viongozi wengine katika kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za Sensa katika Wilaya sambamba na kuhakikisha kuwa Elimu kwa Wananchi inatolewa ipasavyo.
Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Semina ya Wajumbe wa Baraza hilo iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Balozi Seif ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Taifa ya Sensa Tanzania alisema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni Miongoni mwa Wajumbe wa Kamati za Sensa za Wilaya.
Alisema ni vyema wakatumia nafasi zao kama Wawakilishi wa Wananchi kuhamasisha na kuelimisha Umma kuhusu umuhimu wa kushirikiana na Makarani wa Sensa wakati wa kipindi cha kuhesabu kwa kutoa Takwimu sahihi.
Alifahamisha kwamba hatua hiyo itasaidia kupata Taarifa kwa ajili ya Mipango ya Maendeleo. Balozi Seif alieleza kwamba Serikali hutumia Takwimu zitokanazo na Sensa katika kutunga Sera, kufanya maamuzi juu ya Utawala wa Umma kwa kuzingatia mahitaji halisi pamoja na vigezo vya umri na Jinsia.
“ Sensa ya Mwaka huu wa 2012 ina umuhimu wa kipekee kwa kuwa Taarifa zitakazokusanywa zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa dira za Taifa za Maendeleo za Mwaka 2025 Upande wa Bara na Mwaka 2020 kwa Upande wa Zanzibar”. Alisisitiza Balozi Seif.
Mwenyekiti huyo Mwensa wa Kamati ya Tifa ya Sensa Tanzania aliongeza kuwa Takwimu hizo zitatumika pia kutathmini Utekelezaji wa Malengo ya Milenia ifikapo Mwaka 2015 na Ule Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano wa Mwaka 2011/12 hadi 2015/16.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Mh. Omar Yussuf Mzee alisema Wajumbe wa Baraza hilo ambao watakuwa wajumbe wa Kamati za Sensa katika maeneo yao wataendelea kupata muendelezo wa Semina za mara kwa mara kwa kuhusiana na Masuala ya Sensa ya Watu na Makazi.
Mh. Omar alifahamisha kwamba nia ya kutolewa kwa Taaluma hiyo mara kwa mara kwa Wajumbe hao imelenga kuhakikisha kila mwana Jamii anaelewa na kutambua jukumu lake katika kuhakikisha Sensa ijayo inafanikiwa vyema.
Akizuingumzia Madodoso yaliyotayarishwa Waziri Omar alieleza kwamba Serikali imeamuwa kuwa na Dodoso la Jamii ambalo litafanyiwa kazi kwa mara ya kwanza ndani ya zoezi hilo la Sensa.
Alisema mapango unakusudiwa kufanywa kwa tathmini ya hali ya mazingira katika maeneo mbali mbali hapa nchini. Masuala 62 yanatarajiwa kuulizwa katika Dodoso refu wakati lile Dodoso fupi litakuwa na Maswali 37.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment