Wasanii Nchini wameaswa kuacha tabia ya kujisikia kupindukia mkapa wakati wanapokuwa tayari wameshakubalika kutokana na kuwasilisha fani yao kwa jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akikabidhi Mchango wa Shilingi Milioni moja {1,000,000/- } kwa Kikundi cha Muziki wa Taarab cha Zanzibar One Taarab hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Mchango huo aliomkabidhi Mkurugenzi wa Kikundi cha Zanzibar One Taarab Abdulla Ali { Du } unafuatia ahadi aliyoitoa Balozi Seif wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Kutimia Miaka Mitano tokea kuanzishwa kwa Kikundi hicho zilizofanyika Katika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar Tarehe 21 Aprili 2012.
Balozi Seif alisema kumekuwa na tabia inayoanza kutoa sura mbaya kwa wapenzi wa Sanaa na Hata Michezo mengine ya kuwalalamikia Wasanii na Wachezaji ambao hufanya kiburi baada ya kujiona wanatajika ndani ya Jamii.
“ Mastaa wetu hasa wale wanaojulikana zaidi na Jamii baadhi yao wamekuwa na tabia ya maringo jambo ambalo halipendezi kwa wapenzi wao. Wanajisahau kwamba wao ni kioo cha Jamii wanatakiwa kuwa mfano bora wa matendo yao ya kila siku” Alisisitiza Balozi Seif.
“ Kwa wenzetu walioendelea hasa Nchi za Ulaya na Bara la Asia Tabia hii imekuwa ni ya kawaida tu, lakini kwa sisi Nchi Maskini na changa tunaochipukia hatujafikia kuwa na hulka hii”. Aliendelea kufafanua zaidi Balozi Seif. Alikemea tabia hiyo kupigwa vita mara moja au vyenginevyo Wasanii na Wanamichezo hao Maarufu wanaweza kujikuta wakitengwa na Wapenza wao.
Balozi Seif aliendelea Kukipongeza Kikundi cha Zanzibar One Taarab kwa juhudi zake za Kutoa Burdani na hata Taaluma kwa Wapenzi na Wananchi kupitia Sanaa hiyo ya Taarab.
Aliwataka Wasanii hao kuendeleza Umoja na kushikamana miongoni mwao wakitambua kwamba bado wana dhamana na wajibu wa kutoa huduma kwa Jamii kupitia fani yao. Akipokea Mchango huo Mkurugenzi wa Kikundi cha Zanzibar One Taarab Ustadhi Abdulla Ali { Du } kwa niaba ya wana Kikundi wenzake alimshukuru Balozi Seif kwa kutekeleza ahadi yake ndani ya kipindi kifupi.
Mkurugenzi Du alisema Mchango wa Balozi Seif hasa wakati huu kwa kiasi kikubwa umekuwa chachu ya kukisogeza Kikundi chao katika hatua ya mafanikio zaidi. Abdulla Ali Alimuhakikishia Balozi Sei kwamba mchango huo uliokuja kwa wakati muwafaka utatumiwa kwa lengo la kukinufaisha zaidi Kikundi na Wasanii wake wote.
Kikundi cha Zanzibar One Taarabu kilichoanzishwa Mwaka 2007 hapa Zanzibar chini ya Mlezi wake Ustaadhi Mohd Ahmed kikiwa na Wasanii 18 miongoni mwao wanane ni wanawake kimelenga kutoa burdani kwa njia ya Taarab ya Kisasa. { Modern Taarab }.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top