India imeombwa kuongeza nafasi zaidi za Masomo ya juu kwa Wanafunzi wa Zanzibar katika kuwapatia Elimu itakayokidhi soko la ushindani litalosaidia kuimarika kwa Uchumi wa Zanzibar.
Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Balozi Mdogo wa India hapa Zanzibar Bw. D. S. Singal aliyekwenda kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa Utumishi hapa Zanzibar hapo Ofisini kwake katika Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni.
Balozi Seif alisema Zanzibar imekuwa ikizalisha kundi kubwa la Wanafunzi wanaomaliza masomo yao ya Kidato cha Sita kila mwaka. Hivyo India inaweza kutumia fursa hiyo kusaidia kuwaongezea Taaluma Vijana hao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi Singal kwamba Zanzibar bado ina Wataalamu hafifu ambao inahitajika kuongezewa nguvu za ziada.
Balozi Seif alimpongeza Bwana Singal kwa utumishi wake mzuri hapa Zanzibar uliopelekea kuimarisha uhusiano zaidi kati ya Zanzibar na India hasa katika masuala ya Elimu na Afya.
Alisema India imekuwa ikisaidia kwa kina huduma za matibabu kwa wagonjwa wa Zanzibar na kuitaka iendelee na mpango wake huo sambamba na kutoa Taaluma kwa Madaktari wa Kizalendo kupata mafunzo nchini humo.
Akizungumzia suala la Viwanda Vidogo vidogo Balozi Seif alimueleza Balozi Singal kwamba India ina nafasi kubwa ya kuwekeza katika eneo hilo kwa vile imeshapiga hatua zaidi ya Kiteknolojia katika sekta ya Viwanda.
Alisema Zanzibar imekuwa na mali ghafi nyingi hasa za kilimo na kupelekea bidhaa zake kukosa hifadhi na hata soko la kimataifa kutokana na ukosefu wa viwanda vya usindikaji kitaalamu.
Mapema Balozi Mdogo wa India anayemaliza muda wake hapa Zanzibar Bwana Singal ameelezea faraja yake kutokana na kujifunza mengi wakati wa utumishi wake hapa Zanzibar.
Balozi Singal alisema maisha ya pamoja yanayoendelea kudumishwa ndani ya Visiwa vya Zanzibar kupitia mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa umetoa changamoto kwa mataifa mengi kuiga mfano huo.
Alisema Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa za Maendeleo katika kipindi kifupi kutokana na utulivu wa Kisiasa uliopo miongoni mwa Wananchi wake.
Balozi Singal alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba India itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika masuala ya Elimu na Afya.
Alisema Mpango wa India wa kufikiria kuanzisha Mafunzo ya Amali hapa Nchini itapewa msukumo sambamba na ule Mpango uliopo wa Ushirikiano baina ya India na Bara la Afrika.
Balozi Singal amemaliza muda wake wa utumishi Hapa Zanzibar ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita. Taaluma ya mawasiliano ambayo tayari taratibu zake zimeshaanza kuchukuliwa pia
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top