Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi amewataka Wanachama wa Umoja wa Wapanda Mapiki Piki wa CCM kufanya maamuzi Magumu lakini ya Busara katika kuhakikisha wanachagua Viongozi bora kwa ajili ya kujenga safu ya Ushindi wa chama hicho kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Ametoa wito huo katika Mkutano Mkuu wa Umoja huo uliokutana kufanya Uchaguizi wa Viongozi wake watakaoongoza Umoja huo katika kipindi cha Miaka mitano ijayo hapo katika Ukumbi wa CCM Mkoa Amani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema CCM iliwahi kupata uvamizi ndani ya Jumuiya na Baadhi ya Taasisi zake na hatimaye kupelekea Matatizo hasa katika chaguzi zilizopita.
Alitahadharisha kwamba wakati umefika kwa Wanachama wa Chama hicho kuwa makini na watu kama hao hasa katika kipindi hichi kinachoingia cha chaguzi mbali mbali za Viongozi wa Chama hicho.
“ CCM haioni shida kupoteza wanachama watatu, watano ambao wana tabia na njama za kukidhoofisha Chama kwa maslahi yao binafsi”. Alisema Balozi Seif.
Balozi Seif amewaomba Vijana hao kujisaidia katika kuachana na mifarakano kwa lengo la kutengeneza safu nzuri ya muelekeo bora wa Uongozi makin.
Akiwapongeza Vijana hao Balozi Seif aliwaomba kuendelea kukiimarisha Chama chao kwani wao ndio nguvu ya Chama wakati wote.
Balozi Seif ameahidi kwamba kwa kushirikiana na mlezi wa Umoja huo ataangalia hatua za namna ya kuisaidia Taasisi hiyo muhimu kwa CCM katika masuala ya uhamasishaji Wanachama.
Katika Taarifa yao iliyosomwa na Katibu wa Umoja huo wa wapanda Mapiki Piki Mkoa Mjini Magharibi Nd. Amour Ali Mwinyi amesema Umoja huo umepata mafanikio makubwa tokea kuanzishwa kwake.
Hata hivyo Nd. Amour alisema Taasisi yao bado inakabiliwa na baadhi ya changamoto zinazokwaza utendaji wao ikiwa ni pamoja na msingi wa kianzio cha kuelekea katika uzalishaji mali.
Mapema Mlezi wa Umoja wa Wapanda Mapiki Piki Mama Asha Suleiman Iddi amempongeza Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Sheni kwa jitihada zake za kuunga mkono umoja huo.
Mama Asha ameziasa Taasisi za CCM zinazoingia kwenye uchaguzi kuwachagua Viongozi wao kwa kigezo cha Uwezo na kuachana na tabia ya kuangalia udugu au rafiki.
Alisema tabia hiyo ikiendekezwa inaweza kukijengea mazingira mabovu Chama katika utekelezaji wa Sera na Majukumu iliyojipangia ndani ya Ilani yake.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment