Viongozi na Watendaji wa Serikali wanapaswa kuendelea kushajiisha Jamii ili kuepuka athari za Mazingira zinazotokana na Baadhi ya Watu kuwa na tabia ya kuchimba Mchanga katika maeneo yenye rutba inayoweza kuotesha mazao mbali mbali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli hiyo baada ya kulikagua eneo lililokatwa Minazi kwa dhamira ya kutaka kuchimbwa Mchanga katika Kijiji cha Bumbwini akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya Maendeleo na ile ya Kijamii ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Zipo dalili zinazoonyesha baadhi ya Watu wanajiandaa na mpango wa kutaka kuendesha zoezi la Uchimbaji wa Mchanga licha ya amri iliyotolewa na Waziri Kiongozi Mstaafu kuzuia kabisa uchimbaji huo miaka michache iliyopita. Balozi Seif alisema Maafisa wa Misitu lazima wawe wakali wakati wote vyengine Taifa linaweza kuangamia kutokana na baadhi ya watu kuharibu mazingira kwa kisingizio cha kujitafutia Maisha.
Aliwapongeza Wananchi wa Kijiji cha Bumbwini kwa msimamo wao wa kuzuia zoezi la uchimbaji mchanga kwenye eneo hilo ambalo bado linaonekana kuwa na rutba ya kuendelezwa shughuli za Kilimo. “ Lengo la Serikali ni kugawa Eka tatu tatu ili Wananchi wapate fursa ya kuendesha Maisha yao katika masuala ya Kilimo na tabia ya kuuzwa Eka hizo ni kwenda kinyume la lengo hilo”. Alitahadharisha Balozi Seif. Mapema Afisa Misitu anayeshughulikia Mapato na Mashamba yote ya Serikali Nd. Mwinjuma Muharami alisema kibali cha kuruhusu uchimbwaji wa mchanga hutolewa baada ya uhakiki wa kuliona eneo husika kama halina uwezo wa uzalishaji wa mazao unaofanywa kwa pamoja na wawakilishi kutoka Taasisi za Misitu, Mazingira, Masheha, Halmashauri, pamoja na Wilaya husika .
Nd. Mwinjuma pia alisema Mpango Maalum umeandaliwa wa kuoteshwa Miti ya kudumu katika Maeneo yote yaliyochimbwa Mchanga kwa lengo la kuhifadhi Mazingira na kurejesha haiba ya Maeneo hayo. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea furaha yake kutokana na kazi nzuri inayofanywa na wana Mazingira wa Jumuiya ya Mabwana na Mabibi Misitu wa Vijiji Saba vinavyojumuisha Hifadhi ya Mikoko ya Ghuba ya Bumbwini Mkokotoni.
Balozi Seif alielezea furaha hiyo baada ya kuweka jiwe la Msingi la Jengo jipya la Hifadhi ya Mikoko katika Ghuba hiyo kwenye kijiji cha Mafufuni Bumbwini. Alisema shughuli za mazingira hivi sasa ni muhimu Duniani kutokana na athari zilizojitokeza ambazo zinaashiria kuleta balaa katika baadhi ya Mataifa Duniani.
Aliwaeleza Wana Mazingira hao kwamba Serikali itaangalia uwezekano wa kuwasiliana na Taasisi na Washirika wa Maendeleo ndani na Nje ya Nchi kuona changa moto zinazowakabiliWana Mazingira hao zinapatiwa ufumbuzi.
Balozi Seif aliweka jiwe la Msingi la Jengo Jipya la Skuli ya Upenja na kuipongeza Kamati ya Skuli hiyo kwa juhudi zake za kuipa thamani kubwa Elimu kwa kuwajengea mazingira Bora Watoto wao. Aliwaasa Wanafunzi wa Skuli hiyo kuzitumia vyema juhudi za Wazazi wao huku Serikali ikijipanga kuunganisha nguvu na Kamati za Maskuli katika jitihada za kuyakamilisha Majengo mapya ya Skuli.
Mapema wakitoa Taarifa fupi ya Skuli hiyo iliyosomwa na Mwalimu Mtumwa Rashid walisema ifunyu wa Maabara, Maji safi na Uhaba wa Madarasa ni miongoni mwa Changamoto zinazoikabili Skuli hiyo iliyopo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.
Balozi Seif akiwa pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alilitembelea Tawi la CCM Mafufuni Bumbwini na kuahidi kutoa Mabati yote ya kuezekea. Akisalimiana na Wana CCM wa Tawi hilo Balozi Seif alisema haoni fahari kuona shughuli za chama cha Mapinduzi zinafanyiwa chini ya Miembe.
Balozi Seif aliangalia ujenzi wa Jengo la Umoja wa Wanawake Tanzania {UWT } Wilaya ya Kaskazini “B” liliopo Mahonda , akakagua Jengo la Afisi Kuu ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja liliopo Mahonda na baadaye aliweka Jiwe la Msingi la Tawi la CCM Donge Kitaluni na kumaliza ziara yake kwa kulifungua Tawi Jipya la CCM Kirombero lililojengwa kwa nguvu za Wanachama wenyewe, Viongozi na Wahisani wa Chama hicho. Akizungumza katika Mikutano hiyo tofauti Balozi Seif aliahidi kutoa mchango wa Shilingi Milioni Moja kusaidia umaliziaji wa Tawi la Kitaluni na Matofali 1000 kwa ajili ya Kituo cha Malezi cha Kijiji hicho cha Donge Kitaluni. Pia aliahidi kutekeleza ahadi yake ya mbao za madirisha yote pamoja na gharama za Huduma ya umeme kwa Tawi la CCM la kirombero.
Balozi Seif alisema na kusisitiza kwamba Matawi ya Chama cha Mapinduzi lazima yawe na Vianzio vya Mapato kwa dhamira ya kuwepuka tegemezi ambayo inawezan kudhoofisha nguvu za Chama.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimaliza ziara yake kwa kukagua eneo linalotarajiwa kuoteshwa Miti ya Matunda na Kilimo mchanganyiko la Bwana Ahmed Talib liliopo Kirombero Wilaya ya Kaskazini “B”. Balozi Seif alimuagiza Mmiliki huyo kushirikiana kwa karibu na Uongozi wa Wilaya ya Kaskazini “B” na Mkoa wa Kaskazini Unguja katika kuona Mradi huo unafanikiwa na kutoa ajira kwa Vijana.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top