Kwa kipindi kirefu mno, ugonjwa wa kifua kikuu haujapewa usikivu wa kutosha. Matokeo ya kutokujali huku ni kuwepo kwa mateso ambayo hayakutakiwa yawepo: Mnamo mwaka 2010 pekee, takriban watu milioni tisa walipatwa na maradhi ya kifua kikuu ambapo watu milioni 1.4 miongoni mwao walifariki, huku asilimia 95 ya vifo hivyo vikitokea katika nchi zinazoendelea. Tarakimu hizi zinaufanya ugonjwa wa kifua kikuu kuwa  ugonjwa ambukizi nambari mbili kwa mauaji ulimwenguni.  
Mawimbi ya madhara haya yanakwenda mbali zaidi ya wale walioathirika moja kwa moja. Kifua Kikuu husababisha kipigo kikubwa kwa familia na jumuiya mbalimbali. Mamilioni ya watoto wamepoteza wazazi. Watoto waishio na wanafamilia walioathirika wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na ugonjwa huo. Isitoshe, wengi wao hawatibiwi, kwa vile si rahisi kuthibitisha uwepo wa maradhi hayo kwenye mwili wa mgonjwa. Kwa hiyo, mwaka huu tunakusudia kupanua uelewa wa jinsi ambavyo watoto huathiriwa na ugonjwa huu.
Ni muhimu kuwasaidia wale ambao hawana nyenzo za kukabiliana nao kwa kuwapa huduma na matibabu ili wafaidi maisha ya afya na yenye kuzaa matunda. 
Twaweza kuleta mabadiliko makubwa iwapo tutachukua hatua zinazofaa. Tunafahamu jinsi ya kuangamiza aina zote za kifua kikuu, hata kile ambacho ni sugu—kilichojitokeza katika nchi nyingi mno—kabla hakijadhihirisha dalili ambazo hutibika kwa gharama kubwa na kuleta mateso ya ziada. Pale ambapo tumechukua hatua za dhati na za uhakika, idadi ya waathirika imepungua kwa kiasi kikubwa.
Shirika la Afya Duniani linaarifu kuwa juhudi zetu za pamoja zimesaidia kupunguza vifo kwa asilimia 40 tangu mwaka 1990. Watu milioni 46 wameponywa kuanzia mwaka 1995 kutokana na juhudi za Umoja wa Mataifa, serikali mbalimbali, wafadhili, makundi ya kijamii, washirika binafsi, wataalamu wa afya, na makumi ya maelfu ya watumishi wa idara za afya pamoja na familia na jumuiya zilizoathirika. Kwa hiyo huu ni wakati muafaka wa kuwa na hamasa kubwa zaidi ya
“Kukomesha Kifua Kikuu katika siku za uhai wetu,” ikiwa ni kauli mbiu wa mwaka huu ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani. Natoa wito wa kuwepo kwa mshikamano wa kimataifa utakaohakikisha kuwa watu wote wanawekwa huru dhidi ya hofu ya kuambukizwa kifua kikuu na kukumbwa na matokeo yake ya kutisha. Yatupasa tukomeshe upuuziaji wa ugonjwa wa kifua kikuu ili kusitisha vifo vitokanavyo na ugonjwa huu katika enzi zetu.

0 comments:

 
Top