Kampuni ya Ujenzi ya Electric International Company Limited imeagizwa kukamilisha ujenzi wa Skuli Mpya ya Sekondari ya Wilaya ya Kusini iliyopo Paje Mtule ndani ya kipindi cha miezi minne vyenginevyo itafukuzwa na italazimika kulipa gharama zote zitakazojiri kuitia hasara serikali.
Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati alipoikagua Skuli hiyo akiwa katika ziara ya Siku moja ndani ya Wilaya ya Kusini kuangalia Shughuli za Maendeleo na Miradi ya Jamii.
Balozi Seif alimuagiza Msimamizi wa Ujenzi huo kwamba Mwishoni mwa Mwezi wa Julai mwaka huu ahakikishe ahadi aliyoitoa anaitekeleza kinyume na hivyo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali italazimika kuifutia mara moja Mkataba wa Ujenzi Kampuni hiyo.
Alisema kitendo cha Makandarasi wa Ujenzi huo kumuahidi rais wa Zanzibar kwamba watakamilisha kwa wakati uliopangwa ujenzi wa Skuli hiyo kimeitia aibu Serikali.
“ Inasikitisha kuona Kiongozi Mkuu wa Kampuni hiyo ya Electric International Company Limited yumo katika Bodi ya Wakandarasi Tanzania. Si dhani kuwa utumbo kama huu tunaweza kuuvumilia” Alikemea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif aliiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha kwamba Mkandarasi huyo anakabidhi jengo hilo katika muda alioahidi.
Alisema kumalizika kwa Skuli hiyo kutasaidia kuondosha upungufu wa Skuli za Sekondari Wilayani ambao wengi wa Wanafunzi wake hulazimika kufuata Elimu ya juu sehemu za Mijini.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Wiara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Abdulla Mzee Abdulla alimueleza Balozi Seif kwamba Ujenzi wa Skuli hiyo ya Baje Mtule umeanza mapema mwaka 2006 kuliko Skuli nyengine zilizomo ndani ya Mradi huo ambazo tayari hivi sasa zimeshakamilika ujenzi wake.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika ziara hiyo aliweka Jiwe la Msingi la Skuli ya Jamii ya Bwejuu {Charity School } ambayo imejengwa kwa nguvu za wahisani na Wananchi wenyewe.
Akizungumza na Walimu, Wazazi, Kamati ya Skuli na Wanafunzi wa Skuli hiyo wapatao 264 wa Maandalizi na Msingi Balozi Seif aliwapongeza Wazazi kwa uamuzi wao wa kuwatengenezea hatma njema ya Elimu Watoto wao.
Alisema Mkoa wa Kusini Unguja umekuwa na Historia ya kutoa Wataalamu wengi Nchini kufuatia misingi imara uliopo kwa kipindi kirefu ya kujenga mazingira bora ya upatikanaji wa Elimu.
Balozi Seif alihamasika na kuahidi kuchangia Shilingi 1,000,000/- kusaidia uendelezaji wa Skuli hiyo iliyogharimu zaidi ya Shilingi Milioni Mia Tisa Nukta Tisa { 994,000,000/- }.
Akilitembelea Jengo la Ofisi ya Elimu liliopo Makundichi Wilaya ya Kusini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema uamuzi wa Watendaji hao wa Elimu Wilayani humo kujijengea Makazi ya kisasa unafaa kupongezwa na kuungwa mkono.Balozi Seif katika kuunga mkono jitihada hizo ameahidi kuchangia Matofali 3,000 na Saruji Mifuko 30 ili kusaidia kukamilisha ujenzi wa Jengo hilo ili kukabidhiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa hatua za uwezekaji.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top