Katika miongo ijayo, suala la kuulisha umma wa ulimwengu na kuhakikisha usalama wa chakula kwa wote litategemea ongezeko la uzalishaji wa chakula. Hii inamaanisha ni lazima kuhakikisha kuwepo kwa matumizi endelevu ya rasilimali muhimu kabisa yenye kikomo—maji.
Ujumbe muhimu wa mwaka huu wa Siku ya Maji Duniani ni ‘ maji na usalama wa chakula’. Kilimo ndicho kinachotumia zaidi maji. Hivyo tusipoongeza kiwango chetu cha kutumia maji kwa uangalifu katika shughuli za kilimo, tutashindwa kumaliza baa la njaa, na kutoa fursa ya kupata matatizo mengine ikiwamo ukame, njaa na vurugu za kisiasa.
Katika sehemu mbalimbali ulimwenguni, uhaba wa maji unaongezeka huku uzalishaji wa kilimo ukipungua. Aghalabu, mabadiliko ya tabia nchi yamezidisha
hatari ya kupata hasara na hali ya wakulima kutokuwa na matarajio ya uhakika, hususan kwa wakulima masikini katika nchi za kipato cha chini ambao ndio hasa wanakabiliwa na tishio hili huku wakiwa na uwezo mdogo wa kukabiliana na hali hiyo.
Changamoto hizi zinazoingiliana zimeongeza ushindani miongoni mwa jumuiya na nchi katika kupata rasilimali adimu ya maji, na kuchochea matatizo ya kale ya usalama na kuzalisha matatizo mengine, hivyo kuweka vikwazo katika upatikanaji wa haki za msingi za binadamu za kupata chakula, maji, na usafi.
Kukiwepo takriban watu bilioni moja wenye njaa na milioni 800 wanaokosa maji biladia, yapo mengi tunayopaswa kufanya ili kuimarisha misingi ya utulivu katika ngazi mahalia, kitaifa na kimataifa. Kuhakikisha kuwepo kwa usalama endelevu wa chakula na maji kwa wote kunahitaji uhusishwaji wa wadau na sekta zote. Jukumu hilo litajumuisha uhamishaji wa teknolojia mahsusi ya maji, uwezeshaji wa wazalishaji wadogowadogo wa chakula na uhifadhi wa huduma muhimu za mazingira. Vilevile utahitaji sera zinazohamasisha haki ya maji kwa wote, uwezo mkubwa zaidi wa usimamizi na usawa wa kijinsia.
Uwekezaji katika miundombinu ya maji, maendeleo ya vijiji na matumizi bora ya maji utakuwa jambo muhimu kabisa. Sote tunapaswa kutiwa nguvu na mwamko mpya ya wanasiasa kuhusiana na usalama wa chakula, kama inavyodhihirishwa na umuhimu wa hali ya juu uliopewa suala hili kwenye ajenda za nchi za G8 na G20, pia mkazo unaojumuisha masuala ya chakula, maji na nishati kwenye ripoti yangu kwa Jopo nililoliteua la Dunia Endelevu, na kuongezeka kwa nchi zinazojiunga na Mpango wa Kukuza na Kuimarisha Lishe.
Katika Siku hii ya Maji Duniani, nawasihi washirika wote waitumie kikamilifu fursa inayotolewa na kuwepo kwa mkutano wa Rio+20 wa Maendeleo Endelevu. Huko Rio, tutahitaji kuunganisha nukta ndogondogo zilizopo baina ya usalama wa maji, chakula na lishe katika muktadha wa uchumi wa kijani. Maji yatakuwa na jukumu kubwa katika kujenga dunia tuitakayo.
0 comments:
Post a Comment