Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Avic ya Nchini China Bwana Xiong Tao akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kuhusu mpango wao wa kusaidia mafunzo ya amali kwa Vijana wa Zanzibar
Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na utoaji wa mafunzo ya    amali na Ufundi Nchini China { Avic Inaternational } inakusudia kuelekeza nguvu zake hapa Zanzibar katiza suala zima la kusaidia soko la ajira kwa kundi kubwa la vijana wanaomaliza masomo yao.
Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo Bwana Xiong Tao ameeleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Xiong  ambae amevutiwa sana na mazingira mazuri aliyoyaona hapa Zanzibar amesema Taasisi yake imekusudia kutoa mafunzo ya Ufundi na Amali kwa Vijana katika dhana nzima ya kuwaejengea  uwezo wa kujitegemea wamalizapo masomo yao.Alisema Avic International hivi sasa inaendeleza mpango wa  kuwapatia mafunzo vijana katika Mataifa ya Zambia na Kenya katika fani ya ufundi.
“ Wakati tunajiandaa na muelekeo wa kutoa mafunzo kwa Nchi za Misri, Tanzania, Zimbabwe, Ethiopia na Eritrea mtazamo wetu wa kwanza Tunaiangalia zaidi Zanzibar” Alisisitiza Bwana Xiong.
Akigusia suala la Kilimo na Utalii Bwana Xiong alimueleza Balozi Seif kwamba Mkazo utawekwa pia na Kampuni yake katika Kutoa Taaluma kwa Wakulima wa Kipato cha chini ili kuwajengea uwezo wa uzalishaji hasa katika Kilimo cha Mpunga.
Alisema yapo mafanikio makubwa kwa wakulima wadogo katika Mataifa mbali mbali ambao hutumia taaluma katika uzalishaji unaowaongezea kipato mara mbili zaidi.
Kuhusu Utalii Bwana Xiong alisema uwezo wa Kampuni yake kutoa mafunzo kwa Vijana katika masuala ya Hoteli unawezekana kinachohitajika ni kuandaliwa mipango ya kutekeleza suala hilo.
Alifahamisha kwamba kufaulu kwa mpango huo kutapunguza wimbi la Wafanyakazi wa Kigeni katika  hoteli za  Zanzibar kwa kisingizio cha ukosefu wa Taaluma kwa Vijana wa Zanzibar.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wazo la Uongozi wa Kampuni hiyo hasa katika masuala ya Amali limekuja wakati muwafaka.
Balozi Seif alisema Zanzibar imekuwa ikizalisha kundi kubwa la vijana wanaomaliza Masomo yao ya Sekondari ambao bado hawajawa na muelekeo wa  uhakika wa  Maisha ya kujitegemea.
Alieleza kwamba hatua hiyo mbali ya kusaidia kuandaa mazingira ya ajira kwa Vijana lakini pia itaisaidia kusukuma uwezo wa Serikali Kuu katika kupunguza watu wasio na ajira.
Kampuni ya Avic International ya China ambayo tayari imeshakuwa na mwakilishi wake Nchini Tanzania imekuwa ikitumia zaidi ya Dola za Kimarekani 15 Bilioni kwenye Bajeti yake ya Mafunzo ya amali Duniani kwa kila mwaka.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top