Taifa limejenga matumaini makubwa ya kupata mafanikio kufuatia Taasisi mbali mbali Nchini kujihusisha na masuala ya Utafiti katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameelezea matumaini hayo wakati akizungumza na Viongozi na baadhi ya watendaji wa Chuo cha Kilimo Kizimbani, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo pamoja na Idara ya Kilimo mara ya kuzitembelea taasisi hizo huko Kizimbani Wilaya ya Magharibi.
Balozi Seif alisema kazi inayoendelea kutekelezwa na Taasisi hizo imejenga matumaini hayo ambayo yanatoa taswira ya melekeo wa mafanikio katika Sekta ya Kilimo Nchini hapo baadaye.
Amesema Maendeleo yoyote lazima yaambatane na Utafiti. Hivyo utaratibu wa Serikali wa kuunda Idara zinazosimamia Mipango, Sera na Utafiti zimelenga katika kujua umuhimu wa Utafiti.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza Vongozi na Watendaji wa Taasisi hizo kwa juhudi zao za kuwaelimisha vijana kwa lengo la kusaidia Wakulima katika maeneo mbali mbali Nchini.
“ Nimefurahishwa sana na kazi zinazofanywa na Kitengo cha utafiti. Kwani mnafanya kazi nzuri, uzuri na ubora wa Taasisi unategemea watendaji. Sifa hii nyinyi mnayo”. Alisema Balozi SeifBalozi Seif amewakumbusha Maafisa wa Kilimo kuwa karibu na wakulima kwa lengo la kufuatilia muelekeo wao wa kilimo ambao unatakiwa kuwa wa kitaalamu zaidi hivi sasa.
Alisema bila ya msaada wao kuna hatari ya wakulima walio wengi kuendelea kuyumba katika uzalishaji mali.
Akizungumzia suala la Chuo cha Kilimo Balozi Seif alisema Serikali itaendelea kujenga mazingira bora zaidi ili kuona kila Kijana mwenye sifa za kujiunga na Chuo anapata fursahiyo.
“ Hatutaki kuona Mwanafunzi ye yote anakosa Elimu kwa sababu ya umaskini wake. Na hii hata Rais mwenyewe Dr. Sheni amekuwa akiisisitiza kila mara ”.Alieleza Balozi Seif.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali asili Nd. Affan Othman Maalim alimueleza Balozi Seif Mikakati ya Wizara hiyo katika kukipa uwezo zaidi chuo cha kilimo Kizimbani .
Nd. Affan alisema Utafiti wa Mazao ya Chakula na hata yale ya Biashara yana lenga kumsaidia kipato Mkulima wa kawaida.
Mapema Mkurugenzi wa Chuo cha Kilimo Kizimbani Nd. Mohd Khamis Rashid alisema chuo hicho kimepata hadhi baada ya kupitishwa kwa Sheria ya kuanzishwa kwake na Baraza la Wawakilishi mwaka 2007.
Nd. Mohd Khamis alisema kufuatia usajili rasmi wa Baraza la Vyuo vya Ufundi Tanzania Mitaala iliyopo hivi sasa imekiwezesha chuo hicho kutoa mafunzo ya Diploma ambapo mkupuo wa mwanzo wa Wanafunzi wake unatarajiwa kuhitimu mwaka 2013.
Alisema chuo hicho chenye Walimu 24 na wafanyakazi 49 kimeshatoa Wahitimu 383 tokea kuanzishwa kwake na hivi sasa kina wanafunzi 155 wa jinsia tofauti.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kukitembelea Chuo cha Kilimo Kizimbani , Maktaba, Jengo la Maabara , Darasa la Kompyuta, Kituo cha Usarifu wa Mazao,Maabara za Wadudu na Maradhi ya mimea pamoja na utafiti wa Udongo, Mazao ya Chakula na biashara.

0 comments:

 
Top