Taifa Limelazimika kujiandaa kutoa fursa kwa Wananchi kutoa Maoni yao kupitia Mfumo wa Tume itakayoundwa na Rais wa Jamuhuri ili kuwapa nafasi ya kutumia Demokrasia yao katika ushiriki halali wa mchakato mzima wa Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika Mkutano wa wadi za Fujoni na Kitope zilizomo ndani ya Jimbo lake wakati akizungumza na Viongozi wa CCM katika dhana ya kutoa taaluma ya kujiandaa na mchakato wa Katiba Mpya uliofanyika hapo Ofisi ya Jimbo Kinduni.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Wananchi wote lazima wapate fursa ya kutoa mawazo yao kwa kina kwa vile Katiba hiyo itaihusu na kuhudumia Jamii yote ya Watanzania.
Aliwataka Viongozi na Wananchi hao kuzingatia jambo la msingi la mfumo wa Taifa hili uliopelekea amani na Utulivu wa Jamii ambao umekuwa mfano Duniani.
Amewatahadharisha Viongozi hao kwamba watapodharau kutoa maoni katika yale masuala ya msingi yaliyowazunguuka ni kujinyima haki yao ambayo walistahiki kuipata.
Akizungumzia suala la uchaguzi wa Chama chao Unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu Balozi Seif aliwakumbusha Viongozi hao kujitayarisha kwa kuwachaguwa Viongozi Makini watakaosimama imara kukipatia ushindi chama hicho katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Kitope Mh. Makame Mshimba Mbarouk alitahadharisha kwamba Katiba ni roho ya Nchi, hivyo ni lazima iheshimiwe na kulindwa ipasavyo.
“ Suala hili la kuelekea kwenye mchakato wa muundo wa Katiba Mpya kamwe si la Kuchezea ”. Alikumbusha Mh. Mshinba.
Mh. Mshimba amewapongeza Wananchi wa Jimbo la Kitope kwa kuitumia vyema fursa yao wakati wa kupiga kura ya maoni wakati wa kutafuta mfumo wa muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Wakitoa mawazo yao Baadhi ya Viongozi hao walisema taaluma ya msingi inahitajika kwa Wananchi waliowengi ili kuhakikisha mchakato huo unafanikiwa kama ilivyokusudiwa.
Walisema lipo kundi kubwa la Wananchi ambao hata Katiba iliyopo hivi sasa ambayo inahitajika kufanyiwa marekebisho hawaielewi jambo ambalo si vyema likaachiwa.
Balozi Seif amekutana na Viongozi wa Wadi za Fujoni na Kitope zilizojumuisha Matawi 12 katika ziara za kutoa elimu juu ya muelekeo wa kujiandaa na matayarisho ya utoaji wa Maoni kuhusu Katiba mpya ya Muungano wakati utakapowadia.
Utoaji huo wa Maoni utanza mara baada ya aRais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuteua tume itakayoratibu na kukusanya Maoni hayo ya Wananchi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top