Wajasiri amali walioanzisha soko la Jumapili wametakiwa kuhakikisha kwamba azma yao waliyoibuni na kuianzisha wanaendelea kuifanyia kazi na kuitekeleza kama Ilivyokusudiwa.
Hatua hiyo itawasaidia kujenga hatma njema ya maisha yao katika mazingira ya kujiwezesha kiuchumi kutakaopelekea kujikimu kimaisha na kupunguza umasikini.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akilizindua rasmi soko la Jumapili { Sunday Market } hapo katika uwanja wa Kisonge Michenzani Mjini Zanzibar.
Soko hilo litakalowajumuisha wajasiri amali mbali mbali Mjini na Vijijini litakuwa likitoa huduma tofauti ambazo zitakuwa zikizalishwa na Wahasiri amali wenyewe kupitia vikundi vya ushirika na hata mtu mmoja mmoja.
Balozi Seif ambae alipata fursa ya kuangalia bidhaa mbali mbali zinazozalishwa na Wajasiri amali hao zikiwa katika mabanda maalum yaliyoandaliwa ameelezea kufurahishwa kwake na hatua waliyoifikia ambayo inafaa kuendelezwa.
Alisema Sekta ya wajasiri amali ni muhimu katika ustawi wao. Hivyo ni vyema wakajizatiti ili kufanikiwa na kuacha tabia iliyozoeleka ya kuchumia tumbo.
“ Matajiri wengi hapa Nchini walianzia na Biashara ndogo ndogo na hatimae kufikia ufanisi mzuri kwa vile waliweka malengo mapema ”.Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwapongeza Wajasiri amali hao kwa moyo wao wa kijiletea Maendeleo kutokana na soko hilo kuanza vizuri kwa vile wametafuta njia sahihi ya kujiajiri wenyewe.
“ Tunalianza Soko hili leo kwa nguvu mpya, na lazima liendelee kwa nguvu zile zile ”. Alitanabahisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi ameahidi kukizawadia shilingi 500,000/- kikundi cha utamaduni cha wanafunzi wa Kiongoni Makunduchi kutokana na burudani yao safi waliyoitoa kwenye hafla ya uzinduzi wa Soko hilo la Jumapili.
Mapema Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Mh. Haroun Ali Suleiman aliwaomba Wajasiri amali wote wa Mikoani na Wilayani kuitumia Sunday Market kwa vile na wao wana haki na fursa ya kulitumia soko hilo.
Waziri Haroun alisisitiza kwamba bidhaa zote zinazozalishwa na Wajasiri amali hao zinahusika katika Soko hilo la Juma Pili.
Wakisoma Risala yao iliyosomwa na Nd. Saada Haji Hassan Wajasiri amali hao walisema uanzishwaji wa Soko hilo ni faraja kubwa kwao kwa vile kundi kubwa la Jamii hasa Wanawake na Vikjana litapata ajira.
Walisema Sekta ya Wajasiri amali ni eneo kubwa linaloibua vipaji vya wabunifu katika miradi tofauti ya uzalishaji Bidhaa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top