Jumla ya maeneo 3,024 ya kuhesabia Watu { EAs } yametayarishwa kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ikilinganishwa na maeneo 2,062 yaliyotumika katika Sensa ya mwaka 2002.
Mtakwimu mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Nd. Mohd Hafidh alisema hayo wakati akitoa Taarifa ya Maendeleo ya Kazi za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Ukumbi wa Juu wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Nd. Mohd Hafidh alisema kwa upande wa Zanzibar kazi za matayarisho ya upigaji picha angani imeshafanywa na Kitengo cha mradi wa Smole ikienda sambamba na uchoraji ramani.
“ Hatua ya mwisho ni kutumia ramani kwa kuziweka katika mfumo wa picha na hatimaye kutengeneza ramani za maeneo madogo madogo ya kuhesabia Watu ambapo kila eneo linakadiriwa kuwa na idadi ya ya watu 300 hadi 500 kwa wastani wa kaya 60 hadi 100 ”. Alifafanua Mtakwimu Mkuu huyo wa Serikali.
Ndugu Hafidh alieleza kuwa Sensa ya Watu na Makazi ni chanzo muhimu cha Takwimu ambazo hutumika katika kutunga Sera za Kijamii na Kiuchumi kwa kutathmini ubora wa hali za maisha ya watu.
Nd. Hafidh alimueleza Balozi Seif ambaye alikuwa sambamba na Uongozi wa Juu wa Wizara yake katika kikao hicho kwamba Takwimu zitakazokusanywa katika Sensa ya mwaka 2012 zitatumika kutathmini programu mbali mbali za maendeleo kama Mkuza , Mkukuta na Malengo ya Milenia ifikapo mwaka 2015.
Mtakwimu Mkuu huyo wa Serikali alisisitiza kwamba mfumo unaotumika katika utekelezaji wa Sensa za Watu na Makazi kwa Tanzania ni ule wa kuhesabu watu wote waliolala usiku wa kuamkia siku ya sensa katika maeneo yote ya Nchi bila ya kujali uraia wa watu hao.Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameelezea faraja yake kutokana na muelekeo wa mafanikio katika matayarisho hayo ambayo ni muhimu kwa Maendeleo ya Taifa.
Balozi Seif alishauri kwamba uhamasishaji wa Wananchi katika zoezi hilo ni vyema ukafanywa kwa kutumia vyombo vyote vya Habari Nchini.
Aliitaka Kamati ya Sensa kuwatumia Wawakilishi na Wabunge kuwaelimisha Wananchi wao umuhimu wa Sensa kwani wao ndio wenye Watu Majimboni.
“ Wananchi wana tabia ya kupenda kuhoji jambo wanalopelekewa. Sasa itapendeza kuona Elimu ya zoezi la kazi za Sensa inawafikia kwa haraka ”. Alitahadharisha Balozi Seif.
Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 inatarajiwa kuanza usiku wa kuamkia Tarehe 29 mwezi wa nane mwaka huu wa 2012 na kuendelea hadi Tarehe mosi Septemba mwaka huu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top