Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema hatua za Serikali za ujenzi wa Masoko katika maeneo tofauti Nchini imelenga kuwajengea mazingira mazuri wavuvi kujituma kwa ufanisi na hatimae kuchangia Uchumi wa Taifa.
Balozi Seif alisema hayo katika shamra shamra za maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati akiweka jiwe la msingi la Soko la kisasa la Samaki katika Kijiji cha Tumbe kiliopo Wilaya ya Micheweni Mkoa Kusini Pemba.
Alisema Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yalikuwa na azma ya kubadilisha maisha ya wakulima, Wakwezi na Wavuvi kuwa bora zaidi na hii inaonyesha wazi Uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi unatafsiri kwa vitendo azma hiyo.
“Leo hii tunashuhudia azma hii hapa Tumbe. Soko litakalojengwa hapa ni soko lililokusidiwa kumkomboa Mvuvi kutokana na Umaskini ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wavuvu wanaotumia Bandari ya Tumbekuheshimu uhifadhi wa mazingira ya Baharikwa kujiepusha na Uvuvi unaokatazwa.
Alisema Serikali haitegemei hata mara moja Wavuvi wa eneo hilo wakaanza kutumia nyavu zilizokatazwa au kutumia baruti kwa uvuvi. Balozi Seif lisisitiza kuzingatiwa matumizi bora ya rasilmali za bahari ili jamiiiendelee kuzivuna.
“ Mnataka kuvua leo, kesho na keshokutwa. Ukitumia nyenzo zilizokatazwa na unajua yapo mazalia ya Samaki jua kwamba utavua leo tu ”. Alitanabahisha Balozi Seif.
Balozi Seif alisema hakuna sababu Zanzibar isiuze samaki nje ya Nchi endapo miundo mbinu ya Bahari itakamilika kutokana na rasilmali nyingi zilizopo Baharini.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi dr Kassim Gharib alisema bado Wavuvi waliopo Nchini hawajafikia kiwango cha kujikimu licha ya Rasilmali kubwa ya Bahari iliyopo.
Dr. Gharib amesema Wizara ya Mifugona Uvuvi itaendelea kushirikiana na kamati mbali mbali katika maeneo tofauti nchini kwa lengo la kulinda rasilmalihiyomuhimu.
Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuzungumza na Wananchi Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Said Ali Mbarouk alisema Soko la Tumbe ni miongoni mwa Miundombinu ya Bahari inayoendelea kuimarishwa .
Mh. Mbarouk alisema miundo mbinu hiyo inaimarishwa ili kuwapauwezo zaidi wavuvu kuvua katika Bahari kuu kwa lengo lakuongeza ajira na pato lao.
Alifahamisha kwamba Wizara hiyo inaendelea na mazungumzo na washirika wa Maendeleo kwa ajili ya kujenga sehemu maalum ya uingizaji wa boti ndani ya soko hilo { jet } ili kuwepuka tabia ya ubururaji wa amaki ambao umeoeleka katika sehemu mbali mbali za Masoko hapa Nchini.
Soko hilo la kisasa litakalokuwa na sehemu za kunadia samaki, stoo ya hifadh ya samaki, eneo la matengnezo ya boti za wavuvi pamoja na vibanda vya Biashara ya chakula { Maarufu mama ntilie} linatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Bilioni 1,074,808,177 /-.
Takwimu za Wataalamu wa Uvuvi zinaonyesha kwamba Bandari ya Tumbe hupokea Tani 30,000 za samaki kwa mwaka ikitanguliwa na Bandari ya Malindi inayopokea Tani 60,000 za samaki kwa mwaka.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top