Imani ya Wananchi na hata Wawekezaji na wageni wanaoingia Nchini kwa Jeshi la Polisi itaondoka iwapo uadilifu na uaminifu miongoni mwa Askari wa Jeshi hilo hautakuwepo.
Baadhi ya Vituo vya Polisi hasa vile vinavyohudumia wageni mara nyingi vimekuwa vikilalamikiwa kutokana na ucheleweshaji wa huduma zinazotolewa na vituo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiweka jiwe la msingi na ufunguzi wa Nyumba za Polisi katika Kituo cha Jeshi hilo kiliopo katika Kijiji cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja.
Hafla hiyo ni mfululizo wa shamra shamra za maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia miaka 48.
Alisema uadilifu katika vituo vya Polisi unachangia kujenga jina zuri katika Jeshi hilo ambapo raia na Wageni watajenga picha nzuri wkati wanapohitaji huduma kwenye Taasisi hiyo ya Kijamii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amempongeza Bwana Ivan Kodeh wa Kampuni ya Cristal na Bwana Hussein Al Hashim kwa ufadhili wao wa ujenzi wa nyumba hizo za polisi.
Balozi Seif ametoa wito kwa wafadhili wengine kujitokezmaeneo mengine ya kuungana na Serikali katika kuwajengea askari makaazi bora katika maeneo mengine ya Zanzibar kwani bado upo upungufu wa nyumba za askari.
“ Nafarajika kuona ujenzi wa nyumba hizi umechangiwa kwa kiasi kikubwa na wafadhili wenye vitega uchumi wa mahoteli na nyumba za kulala wageni ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Hata hivyo Balozi Seif alisema Serikali itaendelea kujenga makaazi ya wananchi wake vikiwemo Vikosi vya Ulinzi kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo kwa lengo la kuimarisha Makaazi bora.
Alikemea tabia ya kufichwa kwa wahalifu ndani ya Jamii ikaachwa mara moja kwani inachangia ukosefu wa utulivu katika maeneo.
Mapema Kamishna wa Polisi Zanzibar Bwana Mussa Ali Mussa alisema Jeshi hilo kwa kushirikiana na Wawekezaji na Washirika wengine limekuwa likijitahidi kupunguza changamoto zilizopo za uhaba wa Vituo na Nyumba za Askari.
Kamishna Mussa amezipongeza Serikali zote mbili kwa kuendelea kuliimarisha Jeshi hilo kadri uwezo unavyoruhusu.
Ujenzi wa nyumba iliyokamilika ambao umefadhiliwa na Bwana Ivan Kodeh umegharimu Jumla ya Shilingi milioni 45,000,000/- wakati ule unaoendelea liofadhiliwa na Bwana Hussein Al Hashim umefikia shilingi Milioni 37,000,000/- na ameahidi kutoa Dola za Kimarekani elfu 10,000 kuendeleza ujenzi huo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top