Yapo matumaini makubwa ya kuelekea kwenye Maendeleo bora kufuatia kuongezeka kwa nguvu na harakati tofauti za miundombinu zinazofanywa na Serikali kupitia Viongozi wake hapa Nchini.
Kiongozi wa Kanisa la Uamsho Mkuu   Mchungaji Naaman Shauri  alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Hapo Katika Ofisi za Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje Kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mchungaji  Naaman  akiwa na Uongozi wa Juu wa Shirika la Utafiti na Uandishi wa Miradi Tanzania { RPPWA } katika mazungumzo hayo walikuwa wakiangalia namna gani Taasisi zao zinaweza kusaidia  uratibu wa upatikanaji wa Nguvu za Misaada katika Miradi mbali mbali ya Maendeleo ya Jamii hapa Nchini.
Alisema katika kipindi kifupi cha uwepo wa Viongozi hao wa RPPWA Hapa Zanzibar cheche za kuelekea kwenye maendeleo ya Jamii kupitia miradi tofauti zinaonekana kuchomoza kutokana na umadhubuti wa Viongozi wa ngazi za Juu.
“ Spirit nilioishuhudia ya Viongozi wa Juu ndani ya  kipindi kifupi katika kuona miradi ya Wananchi inatekelezeka imenitia moyo na kunipa faraja ”. Alisisitiza Mchungaji Naaman.
Mchungaji Naaman ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua zake inazochukuwa za kuona Ustawi wa Wananchi wake unaendelea  hatua kwa hatua.
Alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba jitihada za ziada zitafanywa ili kuona wawezezaji walioonyesha nia ya kusaidia miradi ya Jamii hasa ya Elimu   wanatekeleza azma yao.  
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema utaratibu uliopo hivi sasa wa Kuwaachia Wananchi wenyewe kuamua Mradi wanaoupendelea ni uamuzi mzuri.
Amesema Jukumu Kuu la Serikali ni kuhakikisha inaratibu vyema mtiririko wa miradi hiyo.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Wawakilishi wa Kampuni inayohusika na usafirishaji wa watalii kutoka Nchini Marekani iitayo Adventure For Singles.
Wawakilishi hao Bibi Suzy Davis na Bwana Terry Pawelko walimueleza Balozi Seif kwamba Kampuni yao inatarajia  kuleta Watalii moja kwa moja kutoka Nchini Marekani kuanzia mwezi ujao.
Bibi Suzy amefurahishwa na mazingira mazuri waliyoyaona hapa Zanzibar na kuelezea matumaini yake ya kuongezeka kwa Watalii kutoka sehemu mbali mbali Duniani.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi aliuomba Uongozi huo wa Adventure For Single kuwa mabalozi wa Marekani katika Kuutangaza Utalii wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Sekta ya Utalii hivi sasa imepewa nafasi kubwa katika kuchangia Uchumi wa Taifa.
Ujio wa Uongozi wa Kampuni ya Adventure for Singles ni Matunda ya Ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Nchini Marekani aliyoifanya Mwezi Octoba mwaka jana ikiwa na  lengo la  kuitangaza Zanzibar kwa wawekezaji wa marekani.
 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top