Wakati Serikali inaendelea kufanya tathmini ya nyumba na mali zilizomo ndani ya eneo jipya kwa ajili ya utanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Zanzibar Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati imeagizwa kutenga eneo kwa lengo la kuwakatia viwanja Wananchi watakaoathirika na zoezi hilo.
Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati alipofanya ziara ya kukagua ramani mpya ya utanuzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema si vyema kwa wananchi hao baada ya kulipya fidia zao wakaanza kuhangaika huku tayari wameshaathirika na zoezi hilo wakati utaratibu wa kuwapatia maeneo unawezekana.
Aliagiza kufanywa kwa utafiti wa watu waliopewa Viwanja katika eneo la Tunguu kwa zaidi ya miaka miwili kama sheria inavyoeleza na kunyang’anywa kama hawajavijenga viwanja hivyo.
Alisema Serikali haitokuwa tayari kuona viwanja hivyo vimekaa tu bila ya kujengwa na upo wajibu wa kupewa watu waliokuwa tayari kuvitumia.
“ Hii tabia ya wanaokata viwanja wakajigaia wenyewe inarejesha nyuma, na siju itakwisha lini? ”. Aliuliza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewaagiza Viongozi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege pamoja na Majimbo jirani yanayouzunguuka Uwanja wa ndege kuwaelimisha Wananchi lengo la Serikali la kutanua kwa Kiwanja cha ndege.
Balozi Seif Alisema utanuzi wa Uwanja wa ndege utaongeza huduma za ufafiri wa anga utakaopelekea kuimarika kwa pato la Taifa kutokana ongezeko la idadi ya Watalii.
Alifahamisha kwamba uchumi utaendelea kukua iwapo taratibu za uwekezaji zinaimarishwa kwa kukaribisha washirika wa Maendeleo.
Mapema Meneja wa Ufundi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege ambae pia ni mkuu wa kitengo cha mazingira Nd. Mzee Abdulla Mzee alimueleza Balozi Seif kwamba Mamlaka hiyo inaendelea kuangalia uhalali wa vielelezo vya wamiliki wa nyumba na mali katika eneo lililopimwa kwa ajili ya utanuzi wa Uwanja huo.Nd. Mzee alisema kwamba thathmini ya awali inaonyesha kwamba zaidi ya nyumba 200 zimo ndani ya eneo hilo jipya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana na Uongozi wa juu wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege,Mkoa mjini Magharibi pamoja na Jimbo la Kiembe Samaki alilitembelea eneo hilo lenye ukubwa wa Square Metre laki 928,268.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amempelekea salamu za Rambi rambi Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Mauungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda Kufuatia Vifo vya Wananchi 20 vilivyosababishwa na mafuriko yaliyoukumba Mkoa wa Daer es salaam.
Balozi Seif alisema amepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa ya vifo vya Wananchi hao, kuharibika kwa mali za Wananchi na wengine 5000 kuyakimbia maeneo yao kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizoleta maafa hayo.
Alisema Wananchi wote wa Zanzibar wapo pamoja nao katika kipindi hichi kigumu cha msiba mkubwa na kuwataka kuwa subra katikam kuwa na nguvu ya kurejesha hali ya maisha ya kawaida kwa Wananchi wote waliopatwa na maafa hayo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top