Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano zaidi kwa Balozi Mdogo Mpya wa Oman aliyepo hapa Zanzibar ili kuona uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya pande hizo mbili unazidi kuimarika.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake vuga wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mdogo mpya wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Mansoor Al- Busaid aliyefika kujitambulisha rasmi.
Balozi Seif alisema Zanzibar na Oman zina Historia ndefu inayofanana kutokana na baadhi ya wananachi wake kupelekea kuingiliana kidamu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Balozi Mansoor kwamba jitihada za makusudi zitafanywa ili kuona kazi zake zinatekelezeka kwa mujibu wa taratibu zinavyoruhusu.
“ Kwa kweli kazi ya Kidiplomasia ni ngumu na kufanikiwa kwake inahitajika nguvu za pamoja zinazohusisha moja kwa moja uongozi wa ngazi za juu wa Nchi husika ”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alimshauri Balozi Mdogo wa Oman kuangalia uwezekano wa Nchi hiyo kusaidia Utaalamu na vifaa katika Sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji maji.
Alisema Oman imeweza kupiga hatua kubwa katika Uzalishaji wa Kilimo kupitia Mfumo huo. Hivyo unaweza pia kusaidia harakati za Kilimo hapa Zanzibar ambapo Wananchi walio wengi wanategemea Sekta hiyo.
Mapema Balozi Mdogo wa Oman hapa Zanzibar Bwana Mansoor Al- Busaid alisema anaendelea kupata faraja kuona uhusiano wa pande hizo mbili unaimarika kila siku.
Balozi Mansoor alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba katika Utumishi wake hapa Zanzibar atasimamia kuona maombi aliyopewa na yale aliyoyakuta yanafanyiwa kazi.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliendelea kupokea mchango wa pole kufuatia ajali ya M.V. Spice Islanders kutoka kwa Watanzania wanaoishi Nchini Zambia.
Mchango huo umewasilishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Tanzania Mh. Mahadhi Juma Maalim.
Akitoa shukrani zake Balozi Seif amesema Watanzania hao wameonyesha kuthamini na kuguswa na tukio hilo licha ya kwamba wako mbali na nyumbani kwao.
Watanzania hao wametoa mchango wa zaidi ya Shilingi milioni moja za Kitanzania {1,118.600/- }.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top