Nguvu za Chama Cha Mapinduzi zitaendelea kuimarika zaidi iwapo kasi ya Umoja wa Vijana wa Chama hicho itakuwa imara wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Kaskazini B Mama Asha Suleiman Iddi alieleza hayo wakati akiufungua Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa Kaskazini Unguja ulioambatana na Semina hapo katika ukumbi wa Jimbo la Kitope uliopo Kinduni.
Mama Asha ambae pia ni Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kasi hiyo itafanikiwa vyema iwapo Vijana hao wataepuka kubabaishwa kitendo ambacho ni hatari kwa muelekeo wa Chama chao.
Alifahamisha kwamba cha kuzingatia hivi sasa ni kuhakikisha Vijana wote wa Umoja huo wanasoma na kuzielewa kanuni za umoja huo ambazo ndizo zitakazowachunga katika kuimarisha maadili ya Chama.
“ Bila ya Vijana wakiwemo pia na akina mama kazi ya chama inakuwa kubwa na ngumu kiutekelezaji ”. Alisisitiza Mama Asha Suleiman Iddi.
Akizungumzia Suala la Uchaguzi Mama Asha aliwakumbusha Vijana kuwasaidia Watu ambao wana uhakika wa kuwa Viongozi Mahiri wa kukiendeleza vyema Chama chao.
Alisema hilo litafanikiwa kama utendaji wao utaepuka migogoro isiyokuwa na msingi inayoambatana na baadhi ya wanaoomba kura kutumia fedha.
“ Mtataeni Kiongozi ye yote asiyefaa hata kama atatoa msaada mkubwa kiasi gain au Rushwa ”. Alitahadharisha Mama Asha.
Mapema Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd. Miradi Khamis Mussa amesema Umoja huo bado unakabiliwa na Changamoto kadhaa ambazo zinahitajika kufanyiwa kazi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top