Mchango uliokusanywa na Wasanii, Wanamichezo pamoja na Wana habari kwa ajili ya Mfuko wa Maafa kufuatia kuzama kwa Meli ya M.V Spice Islanders mwezi Septemba Mwaka huu umewasilishwa kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.Pambano la soka kati ya Timu ya Wasanii na Wanahabari ndilo lililoshajiisha upatikanaji wa mchango huo.
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi ,Uchumi na Ushirika Mh. Haroun Ali Suleiman ambaye alimuwakilisha Balozi Seif Katika Ugeni Rasmi wa Pambano hilo amekabidhi Fedha hizo akiwa pamoja na Wajumbe wa Kamati iliyoundwa kufanikisha Pambano hilo.
Waziri Haroun alimueleza Balozi Seif kwamba Jumla ya Shilingi Milioni Moja na Laki mbili zimepatikana ambazo kati ya Hizo Shilingi laki tatu ni zake Binafsi na Shilingi Laki tatu ni Mchango wa Jimbo la Makunduchi.
Akipokea Mchango Huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewashukuru Wasanii, Wana Habari na Wanamichezo kwa Kuguswa kwao na Tukio la Maafa ya kuzama kwa Meli. Balozi Seif alisema Mchango wa Wasanii, Wanahabari na Wanamichezo utasaidia kuongeza Mfuko wa Maafa.
Amewahakikishia Wananchi kwamba Fedha zilizotolewa na Wahisani mbali mbali kwa ajili ya Mfuko wa Maafa bado hazijatumika kama baadhi ya Watu wanavyofikiria.
“ Fedha hizi bado zipo na wala hazija tumiwa kwani maamuzi ya matumizi hayo yatatolewa na Baraza la Mapinduzi ”. Alisema Balozi Seif Ali Iddi.
Naye katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Zanzibar Donisia Thomas Ameipongeza Serikali kwa kuwa karibu na Vyama na Taasisi za Kijamii hapa Nchini.
Katika pambano hilo Maalum Timu ya Wasanii iliweza kuibuka na Ushindi wa Goli Moja dhidi ya Wana Habari.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top