MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR BALOZI SEIF ALI IDDI  AKIMKABIDHI VIFAA VYA MICHEZO MBUNGE WA VITI MAALUM KUPITIA CHAMA CHA MAPINDUZI MHE, DIANA CHILOLO KUFUATIA AHADI YAKE ALIYOITOA WAKATI WA ZIARA YAKE MKOANI SINGIDA KWA VIJANA WA SHULE ILONGELO ILIYOPO IRAMBA MASHARIKI PICHANI CHUHUDA WA MAKABIDHIANO HAYO NI MAMA ASHA MKE WA BALOZI SEIF IDDI
Vijana wamekumbushwa kuwa makini katika harakati zao za maendeleo pamoja na Maisha ili kuepuka mitego ya kutumiwa na watu wachache wanaopenda kutumia migongo yao katika kujinufaisha kisiasa na kiuchumi.
Kumbusho hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya ccm Balozi Seif Ali Iddi wakati akikabidhi msaada wa Jezi na mipira kwa Timu za Jimbo la Iramba Mashariki hafla iliyofanyika Nyumbani kwake Mjini Dodoma.
Msaada huo wa seti tatu za Jezi na Mipira sita kwa Timu za Soka na Mpira wa Wavu { Netball } amekabidhiwa Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Mh. Dianna Chilolo ili kutekeleza ahadi aliyotowa yeye na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi siku tatu tuu baada ya kufanya ziara ya kuaga kuwa Mlezi wa Mkoa wa Singida.
Balozi Seif alisema ipo tabia ya baadhi ya watu hasa wana siasa kupenda kuwatumia Vijana kwa maslahi yao jambo ambalo hurejesha nyuma maendeleo yao.
Amewatahadharisha Vijana kutokubali kudanganywa na kuwataka kuwa na moyo wa kupenda Masomo huku wakizingatia pia Michezo ambayo hujenga afya zao.
“ Vijana msikubali kudanganywa na ni vyema mkaelekeza nguvu zenu katika masomo na Michezo ili mjenge afya ya miili yenu ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Balozi Seif aliwahakikishia Wananchi wa Singida kwamba ataendelea kushirikiana nao katika masuala ya Maendeleo lichwa ya kwamba amemaliza muda wake wa ulezi katika Mkoa huo.
Akipokea msaada huo mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki Mh. Dianna Chilolo amempongeza Balozi Seif kwa kutekeleza ahadi yake katika muda mfupi usiotarajiwa.
Mh. Dianna alisema kitendo hicho kimewapa moyo wananchi wa Singida na kumtaka Balozi Seif na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi kuendelea na tabia hiyo njema.
“ Huu ni mfano wa pekee aliotuonyesha Balozi Seif. Kwa kweli ni Viongozi wachache wenye Tabia kama hii ya utekelezaji wa ahadi si zaidi ya wiki moja ”.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top