Tanzania itaendelea kuwa ya amani na usalama kufuatia Wananchi wake waliowengi kupenda tabia hiyo licha ya baadhi ya watu wachache kujaribu kuvuruga sifa hiyo ambayo imejijengea Ulimwenguni.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo akiwa katika ziara ya Kuwaaga wana CCM wa Mkoa wa Singida kwenye Mikutano mbali mbali ya Kiwilaya baada ya kumaliza Utumishi wa Kuwa Mlezi wa Mkoa huo Kichama.
Balozi Seif alisema Mshikamano wa Watanzania unaoendelea kuonyeshwa huku wakizingatia umuhimu wa amani umeleta faraja ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki na kuwaomba wananchi kutokubali kuhadaiwa katika kuichezea Amani.
Alisema jamii inapaswa kuyaepuka makundi na baadhi ya watu wanaoshawishi Wananchi na hawa Wanafunzi wa elimu ya Juu kupinga au kufanya Maandamano dhidi ya Serikali kwa lengo la kuvuruga amani ya Nchi.
Aliahidi kwamba CCM bado inapendwa na itaendelea kuwa na nguvu kutokanana na Sera zake, hivyo bila ya Chama hicho amani haitaendelea kuwepo. “ Mtu wa fujo ataendeleaje kuongoza Nchi bila ya fujo ”. Alihoji Balozi Seif Ali Iddi.
Amewaasa wana CCM kuwepuka Makundi ndani ya Chama ambayo wakati mwingi husababishwa na Fedha zinazotolewa na Baadhi ya Wanachama wakati wanapoomba Uongozi. Aliomba kuondoshwa kwa makundi ndani ya chama kwa vile ndio yanayoleta mashimo.
Akizungumzia suala la Mchakato wa Katiba ya Jamukuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Seif aliwaomba Wananchi kutoa Maoni yao wakati utakapowadia wakizingatia zaidi Msimamo utakaotolewa na Chama chao.
Alisema Bunge linaanza kujadili Rasimu ya muswaada wa sheria utakaomuewezesha Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Tume itakayopokea Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka.
“ Mnapaswa kuwa na hadhari na makini na baadhi ya watu wanaoanza kujadili Muundo wa Katiba Mpya wakati hata hiyo tume haijaundwa. Huko ni kupotosha Wananchi ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Balozi Seif Ali Iddi ambaye amefanya ziara ya kuaga katika Wilaya za Iguguno, Ilongero na Singida Mjini ndani ya Mkoa wa Singida anatarajiwa kuripoti rasmi kuwa mlezi Mpya wa CCM Mkoa Mjini Magharibi mnamo tarehe 19/11/2011.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top