MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR BALOZI SEIF ALI IDDI AKIZUNGUMZA NA BALOZI MPYA WA JAPANI NCHINI TANZANIA BW,MASAKI OKADA ALIYEFIKA OFISINI KWAKE VUGA
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameihakikishia Japan kwamba misaada inayotowakwa Tanzania na Zanzibar kwa jumla itaendelea kutekelezwa kama ilivyopangwa.
Balozi Seif ametoa kauli hiyo hapo Ofisini kwake Vuga wakati wa Mazungumzo yake na Balozi Mpya wa Japan Nchini Tanzania Bwana Masaki Okada.
Alisema Misaada ya Nchi hiyo ukiwemo ule mkubwa wa Maji Safi ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi utawawezesha Wananachi na hata Wawekezaji kutumia huduma hiyo kwa ufanisi.
Balozi Seif alimueleza Balozi Masaki kwamba Japan bado ina nafasi kubwa ya kusaidia Maendeleo ya Kilimo, Maji na hata Mafunzo katika Fani tofauti.
Hatua hii itaziwezesha pande hizo mbili kuendeleza kushirikiana katika ile dhana na uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Zanzibar na Japan.
“ Japan imepiga hatua kubwa ya Kitaalamu katika sekta za Kilimo na Taaluma ya Teknolojia ya Kisasa. Hivyo Taaluma hiyo inaweza kusaidia Nchi nyingi hasa za Bara l;a Afrika ambazo zinategemea zaidi Kilimo ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Akizungumzia Uwekezaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanziba inahitaji Wawekezaji Kutoka Nchini Japan katika kuimarisha uchumi wake.
Alisema ni vyema kwa Makampuni na Taasisi za Uwekezaji Nchini Japan zikaangalia uwezekano wa kufungua Miradi yao Zanzibar hasa katika Sekta ya Utalii ambayo hivi sasa ina wawekezaji wengi zaidi kutoka Nchi za Bara la Ulaya.
Kuhusu suala la Usafiri wa Baharini Balozi Seif aliiomba Japan kuangalia uwezekano wa kusaidia mpango wa SMZ wa Upatikanaji wa Meli kwa ajili usafirishaji Wananchi kati ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
Balozi Seif alisema Zanzibar inahitaji Meli mpya kwa ajili ya kutoa huduma za uhakika zitakazoondoa hofu za wananchi ambao kwa sasa wanategemea usafiri wa Boti.
“ Zanzibar inahitaji kuwa na Meli Mpya hivi sasa kwa vile zile zilizonunuwa katika miaka ya 70 zimeshapitwa na wakati ingawa moja ya M.V Mapinduzi tayari imeshauzwa kutokana na uchakavu wake ”. Alifafanua Balozi Seif.
Naye Balozi wa Japan Nchini Tanzania Bwana Masaki Okada alielezea matumaini yake kwamba Makampuni mengi na hata Taaasisi za Huduma Nchini mwake zimeonyesha nia ya kuwekeza Hapa Zanzibar kwa vile Tanzania ni Miongoni mwa Nchi zilizopewa kipaumbele na Japan katika kushajiisha miradi ya Maendeleo.
Balozi Masaki alisema Japani inaiangalia Zanzibar kama mahala pazuri kwa uwekezaji na ni kituo muhimu zaidi kwa Biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Bwana Masaki alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba ombi la Zanzibar la upatikanaji wa Usafiri wa Baharini ataliwasilisha kwa Waziri wa Fedha wa Nchi hiyo kwa ajili ya ufumbuzi unaostahiki .
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment