TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Watanzania wamehimizwa kuendeleza utamaduni wa kushirikiana na kushikamana masuala ambayo ndio nguzo ya umoja na fahari ya utaifa wao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zaznaibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa himizo hilo katika dua ya kuwaombea waliopatwa na maafa katika ajali ya meli ya M.V Spice Islanders iliyosomwa katika viwanja vya chuo cha Kiislamu cha Al-Haramain ilala Mjini Dar es salaam.
Balozi Seif amesema ushirikiano huo umepelekea Jumuiya za Kimataifa kushuhudia jitihada za pamoja za Wananchi zilizoungana na hatimae kuokoa maisha ya watu kadhaa wakati wa ajali ya Meli Hiyo ya M.V Spice Islanders.
Alisema ni jambo la kutia moyo kuona kuwa jamii nzima ya Watanzania kupitia makundi mbali mbali imeguswa na msiba huo na kuamua kuwafariji wale waliopatwa na maafa hayo.
“ Hii inaonyesha dhahiri mshikamano mlionao na kuwa kiasi gain nyote hapa mlivyoguswa na masiba huu mzito uliowapata wenzetu kule Zanzibar ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewanasihi wasafiri kutoa taarifa mara moja kwa mamlaka zinzohusika pale wanapoona hitilafu katika vyombo wanavyosafiri.
Alisema wakati Serikali inaendelea kuimarisha sheria na usimamizi wa usalama wa vyombo vya usafiri ushirikiano mkubwa unahitajika kati ya watoa huduma za usafiri na wasafiri wenyewe. Balozi Seif alisema pande hizo mbili ndizo halizi zinazoelewa mazingira ya vyombo hivyo.
“ Tusiseme Mungu akipenda tutafika. Inawezekana wasifike kwa kudharau hitilafu zinazojitokeza kwenye vyombo hivyo “ Alisema Balozi Seif.
Kisoma Risala Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya dua hiyo Bibi Shamim Khan amewatahadharisha wafiwa wazisiruhusu nyoyo zao kuomboleza kupita kiasi kwani kufanya hivyo ni kumkosoa Muumba.
Alisema watu wema ni wale wanaomuamini Muumba na wakahusiana kutekeleza amri zake alizowateremshia.
“ Waumini wanapaswa muda wote kumtegemea muumba kwani yeye anajua sababu ya kuleta masiba huo ”. Alisema Bibi Shamim Khan.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top