TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anaondoka Nchini leo kuelekea Jamuhuri ya Watu wa China Kuhudhuria Maonyesho ya Viwanda na Biashara Nchini humo.
Balozi Seif ambaye anafuatana na Mkewe Mama Pili Seif Iddi anamuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muunganowa Tanzania Mh. Mizengo Kayanda Peter Pinda.
Katika Maonyesho hayo yanayofanyika katika Mji wa Sichuan ambayo Tanzania imepata mualiko Makamu wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif anafuatana na Ujumbe wa Viongozi saba pamoja na Maafisa wa Taasisi za Muungano na zile za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Viongozi hao ni pamoja na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungazo wa Tanzania Mh. Cyril Chami, Naibu Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar Mh. Thuwaiba Edington Kisasi pamoja na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar akiwa mwakilishi wa jimbo la Micheweni Mh. Subeti Khamis Makame.
Wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mali asili na Mazingira Zanzibar Nd. Afani Othman Maalim, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Nd. Salum Khamis Nassor, Mjumbe wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar { ZCC } Nd. Nassor Ramadhan Dachi pamoja na Mwakilishi mmoja wa Taasisi ya Vitega Uchumi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kurejea Nchini tarehen 23/10/2011.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekutana na Balozi wa Rwanda Nchini Tanzania Bibi Fatma Nyirakobwa.
Katika mazungumzo yao Balozi Fatma ambaye anaaga baada ya kumaliza utumishi wake Nchini Tanzania amesema juhudi za pamoja za Viongozi wa Kisiasa zimeipelekea Zanzibar kuendelea kuwa na Utulivu na amani.
Balozi Fatma ameshauri uhusiano wa Kibiashara uliopo kati ya Rwanda na Zanzibar inafaa uimarishwe na kuendelezwa zaidi.
Naye makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Mataifa ya Kigeni ndani na nje ya Bara la Afrika yanaendelea kujifunza mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa uliopo Zanzibar.
Balozi Seif amesema mfumo wa kisiasa ulipo Zanzibar hivi sasa umepelekea kuondosha joto la Kisiasa ambalo lilikuwa likiiathiri Zanzibar kwa Muda mrefu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameipongeza Rwanda kwa hatua iliyofikia ya kurejesha amani na utulivu uliokosekana kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top