TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Uchimbaji wa mashimo kwa ajili ya utegaji wa samaki { Maarufu Mabombwe } ndani ya Kitongoji cha kwa Mgogo Sipwese katika Kijiji cha Kengeja umepelekea Maji ya Bahari kuvamia na kuhatarisha eneo kubwa la ardhi ambalo hutumiwa kwa shughuli za Maendeleo.
Tabia hiyo mbaya inayofanywa na baadhi ya Watu imechangia uharibifu mkubwa wa mazingira licha ya juhudi zinachochukuliwa na Wananchi wa Kijiji hicho kujenga Tuta kwa ajili ya kuzuia Maji hayo.
Kasi ya maji imekuwa ikipanda hadi katika makaazi ya Wananchi hali ambayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameishuhudia wakati alipofanya ziara ya ghafla kukagua eneo la mikoko lipatalo ekari tatu ambalo limetiwa moto na watu wanaodhaniwa kuwa ni wategaji wa Nyuki.
Mizinga ipatayo 38 ya nyuki kati ya 50 pamoja na Mikoko iliyokuwemo ndani ya shamba hilo la Mkulima Omar Foum Omar inayokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 6,000,000/- imeteketea kwa moto huo. Akizungumza kwa masikitiko Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema hali hiyo inatisha na ni hatari.
Hivyo jitihada za makusudi zinahitajika ili kujaribu kusaidia udhibiti wa uchafuzi wa mazingira.  Balozi Seif mesema uharibifu wa mazingira uliokithiri umechangia kuwakosesha watoto kupata maeneo ya michezo wakati wakulima wanakosa maeneo ya kilimo.  Hata hivyo Balozi Seif amezipongeza jitihada za Idara ya Maingira kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii ambayo kwa kiasi fuilani imesaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Mapema Afisa Mkuu wa Idara ya Mazingira Pemba Ndugu Mwalim Khamis Mwalim amemueleza Balozi Seif kwamba athari hiyo imechangiwa zaidi ya ukataji onyo wa miti pamoja na uchimbaji holela wa mchanga.
Ndugu Mwalimu amewashauri Wananchi wa Kijiji cha Kengeja kuanzisha Kamati za Mazingira pamoja na Polisi Jamii kwa lengo la kusaidia kupambana na vitendo vyote viovu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top