Familia za wananchi waliofariki na kupotea katika ajali ya Meli ya M.V Spice Islanders usiku wa kuamkia Tarehe 10 Septemba mwaka huu wameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kukiimarisha zaidi Kitengo cha Maafa ili kiwe na uwezo kamili wa kutekeleza vyema majukumu yake.
Ushauri huo umetolewa na baadhi ya Familia za watu waliofariki na kupotea wakati wakifarijiwa na Uongozi wa Juu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ukiongozwa na makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.Wafiwa hao wamesema ni vyema kwa Kitengo hicho kikafanya kazi kwa utaratibu uliopangika ili kutoa huduma mara moja wakati yanapoibuka maafa.
“ Inapendeza kuona tunajisaidia wenyewe kwa kukitumia Kitengo chetu wenyewe wakati yanapotokea maafa huku misaada ya dharura itakayokusanywa na taasisi pamoja na mashirika ya misaada inafuata baadaye ” Alisema mmoja wa wafiwa hao Bwana Khamis Juma. Wafiwa hao wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kupitia viongozi wake wa ngazi za juu kwa kuona umuhimu wa kuwatembelea na kuwapa pole .Wamesema kitendo hicho kimewapa faraja na utulivu wa nafsi na kujihisi kwamba msiba huo sio wao pekee kumbe ni wa Taifa zima .
Akitoa mkono wa pole kwa wafiwa hao mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maafa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar.Balozi Seif Ali Iddi ameitaka jamii kuendelea kuziheshimu familia zilizoondokewa na watu wao ikiwa ni ishara ya kuzipa pole.
Balozi Seif amesema kufanya hivyo kutapelekea kuleta hisia kwa wafiwa hao kujihisi kwamba msiba huo ni wa jamii nzima.Uongozi huo wa Serikali unatarajiwa kuendelea na ziara kama hiyo ya kutoa Mkono wa Pole katika mkoa wa kaskazini Unguja.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top