Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwa makini katika kuhakikisha Maisha ya Wananchi wanaotumia usafiri kwa Njia ya Bahari unakuwa salama na wakuaminika.
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wana habari kufuatia tatizo la hitilafu ya kiufundi lililoikumba Meli ya M.V Serengeti iliyokuwa ikijiandaa kusafirisha Abiria kuelekea kisiwani Pemba jana usiku. Balozi Seif Ali Iddi alilazimika kutoa agizo la kuzuiwa kutosafiri kwa meli hiyo baada ya kupata taarifa za hitilafu kwenye chombo hicho hadi hapo kitakapofanyiwa marekebisho.
“ Nimemuamuru Katibu wangu aende Bandarini Kuwasiliana na Wahusika wa Meli hiyo ili chombo hicho kwanza kifanyiwe marekebisho kutokana na tatizo lililojitokeza na baadae ndio kiendelee na safari zake ” Alisema Balozi Seif Ali Iddi .
Makamu wa pili wa Rais Amekemea tabia ya baadhi ya wafanyakazi wa vyombo vya usafiri wa Baharini ya kushutumiwa kuwazuia Wasafiri kuteremka kwenye chombo wakati yanayojitokeza matatizo kwenye chombo wanachosafiria. Balozi Seif Amesema Abiria ana haki na maamuzi ya kuteremka kwenye chombo wakati wowote mradi akishaona kwamba usalama wake uko mashakani.
Amezikumbusha mamlaka zinazoshughulikia usafiri wa njia ya Maji kuhakikisha zinafanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuona vyombo wanavyovisimamia vinafanya shughuli zake kwa njia ya usalama.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kupokea michango kutoka kwa wahisani mbali mbali kusaidia Kamati ya maafa kufuatia ajali ya Meli ya M.V Spice iliyotokea hivi karibuni. Waliotoa michango hiyo ni pamoja na Bodi yaWadhamini wa Mfuko wa Pencheni kwa Watumishi wa Umma Tanzania { PSPF }, jumuiya ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Uongozi wa Kampuni inayosimamia Hoteli tatu za Kitalii za Breeses,Baraza, Palm na Rich son Diving Centre, pamoja na Uongozi wa Kamati ya Mamendeleo ya Kijiji cha kiwengwa.
Wakitoa salamu zao za rambi rambi wawakilishi wa Taasisi hizo wamesema kuguswa na msiba huo ambao ni wa Wananchi wote. Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi amekutana na Balozi wa Israel Nchini Tanzania Bwana Kasbian Nuriel Chirich.
Katika mazungumzo yao Viongozi hao wamezungumzia uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Israel na Zanzibar kwa jumla. Balozi Kasbian amemueleza Balozi Seif kwamba Zanzibar bado ina nafasi kubwa na ya pekee ya kujitangaza kwa Israel hasa katika masuala ya Uwekezaji katika eneo la Utalii na Bahari.
Othman khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top