Habari hii inapatikana kwenye gazeti la Mwananchi tarehe 15.8.2011

Na Fidelis Butahe

SIKU kumi na moja baada ya kutangaza kushusha bei ya mafuta nchini, hatua ambayo ilisababisha mgogoro mkubwa uliotishia uchumi wa nchi, jana Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeongeza tena bei ya nishati hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana Meneja Biashara wa Ewura, Godwin Samwel alisema petroli imepanda kwa Sh 100.34 sawa na asilimia 5.51, dizeli kwa Sh 120.47 sawa na asilimia 6.30 na mafuta ya taa kwa Sh 100.87 sawa na asilimia 5.30 na kwamba bei hizo zitaanza kutumika kuanzia leo.
Alisema bei hizo mpya zimetokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, ikilinganishwa na Dola ya Marekani.
Hatua hiyo ya Ewura imekuja siku moja baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2011/12.
Agosti 3, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu alitangaza bei elekezi iliyoshusha bei ya nishati hiyo ili kumpunguzia makali mwananchi wa kawaida na kusema kwamba petroli ilishuka kwa Sh202.37 kwa lita sawa na asimilia 9.17, dizeli Sh173.49 sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa kwa Sh 181.37, sawa na asilimia 8.70.
Hata hivyo, akitetea uamuzi huo Samwel alisema: “Kulingana na kanuni ya kukokotoa bei ya bidhaa za mafuta ya petroli, bei zimekuwa zikikokotolewa na kutangazwa na Ewura kila baada ya wiki mbili. Bei hizi mpya zimekokotolewa kwa kuzingatia kanuni mpya iliyoanza kutumika mwanzoni mwa mwezi huu.”
Alisema kwamba kwa viwango vya bei hizo mpya, vinaonyesha bei ya nishati hiyo katika soko la dunia vimepanda kwa wastani wa asilimia 5.42, huku thamani ya shilingi ya Tanzania ikiwa imeshuka kwa Sh47.12 sawa na asilimia 2.96 kwa dola moja ya Marekani.
Alisema bei ya jumla na rejareja zingepanda zaidi endapo kanuni ya zamani ingeendelea kutumika... “Kwa kanuni ya zamani, mafuta kwa bei ya rejareja yangeuzwa Sh2,298.33 kwa petroli wakati kwa kanuni mpya sasa ni Sh2,114.12, dizeli ingekuwa Sh2,213.36 wakati sasa ni Sh2,031.31 na mafuta ya taa yangekuwa Sh2,188 wakati wa sasa ni Sh2,005.40,” alisema Samwel. Alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta kwa bei ya ushindani alimradi bei hizo zisivuke ile ya kikomo huku akionya kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei zinazoonekana vizuri.
January Makamba atoa angalizo
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba alitoa angalizo kwa Serikali na Ewura akitaka kuwa makini kuhakikisha taifa halirejei katika uhaba mkubwa wa nishati kama uliowahi kulikumba wiki iliyopita.
Makamba ambaye aliomba Bunge lijadili kwa dharura tatizo la uhaba wa mafuta wiki iliyopita, alisema tatizo kubwa lililopo ni kanuni ya ukokotoaji ya Ewura kutoeleweka vyema kwa wadau. Alisema wakati umefika, kanuni hiyo iwe wazi ili kila mtu ajue inavyotumika hatua ambayo itaondoa malalamiko kwa umma.
“Utaratibu wa ukokotoaji uwe wazi ili kila mtu aujue. Isiwe wanaujua Ewura peke yao, tunachotaka ni kuona industry (tasnia) ya mafuta inatulia. Hatutaki taifa lirudi katika matatizo mengine makubwa ya ukosefu wa nishati ya mafuta. Tusisubiri kuona tena hali kama ile ya uhaba wa mafuta ikijitokeza," alisema.Mnyika aivutia kasi
Kwa upande wake, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amesema atatoa tamko mara baada ya kupitia kwa kina bei hiyo elekezi, lakini akadokeza kuwa ni ishara ya utendaji mbovu wa mamlaka hiyo.“Nitaitolea ufafanuzi kesho (leo), baada ya kupitia bei elekezi…, pamoja na hayo bei hii inanipa shaka ya ufanyaji kazi wa Ewura na Serikali, bei hiyo inaacha maswali mengi sana, huku ni kukosa umakini,” alisema Mnyika
Sakata la Mafuta
Baada ya Ewura kutangaza bei mpya ya mafuta iliyoanza Agosti 3, mwaka huu kampuni zilianza mgomo baridi wa kutouza nishati hiyo katika vituo na kwenye maghala yake hali iliyoilazimu Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura kukutana Agosti 9, mwaka huu na kutoa amri ya kisheria kwa kampuni nne ambazo zilionekana kinara wa mgomo huo BP, Oilcom, Camel Oil na Engen kutoa huduma hiyo mara moja. Baada ya agizo hilo kampuni tatu kati ya hizo zilitii amri hiyo isipokuwa BP ambayo iliendelea na mgomo hatua ambayo iliifanya Bodi hiyo ya Ewura kusitisha leseni ya kampuni hiyo kwa miezi mitatu.Mgomo huo ulisababisha uhaba mkubwa wa mafuta nchini huku walanguzi wakitengeza faida kubwa.

0 comments:

 
Top