CHAMA cha waandishi wa Habari za Michezo Zanzibar (TASWA-ZANZIBAR), kimesikitishwa na taarifa zilizochapishwa katika gazeti la Champion linalotolewa Dar es Salaam toleo la Agosti 8-9, 2011.Katika habari zilizoandikwa na mwandishi Khadija Mngwai na kuchapishwa kwenye ukurasa wa tatu, ilielezwa kuwa, TASWA-ZANZIBAR imeandaa kongamano kubwa la wadau wa michezo wa Unguja na Pemba.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa lengo la kongamano hilo ni kujadili maendeleo ya tasnia ya michezo visiwani humu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.Kwa mujibu wa mwandishi wa habari hizo, taarifa hizo alizipata kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wa TASWA-ZANZIBAR aliyemtaja kwa jina la Hashimu Salim ambaye alisema kuwa kongamano hilo litakuwa la kihistoria na kwamba halijawahi kutokea hapa Zanzibar. Aidha, taarifa hiyo ilifahamisha kuwa suala jengine litakalojadiliwa ni kutokujitokeza kwa wadhamini kukuza soka la Zanzibar, hivyo kupitia kongamano hilo, kutapatikana njia sahihi za kutatua tatizo hilo.
TASWA-ZANZIBAR inapenda kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari, kwamba haijaandaa kongamano hilo wala haijawasiliana na Ofisi ya Rais wa Zanzibar kumuomba awe mgeni rasmi. Halikadhalika, mtu aliyetajwa kuwa ndiye aliyetoa taarifa hizo Hashimu Salim si Makamu Mwenyekiti wa chama chetu wala hana wadhifa wowote ule na TASWA-ZANZIBAR haimtambui. Ni vyema ieleweke kuwa, TASWA-ZANZIBAR ina kamati yake ya uongozi ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kutoa taarifa zake na haitumii watu au mawakala walioko nje ya chama hicho.
Tunapenda ifahamike kuwa taarifa hizo si sahihi, na kwamba mwandishi ameupotosha umma wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.Kupitia taarifa hizi, TASWA-ZANZIBAR inawaomba wananchi na wanamichezo wote wasiziamini taarifa hizo, kwani zimelenga kukichafulia jina chama chetu mbele ya wananchi ambao tayari wameonesha kukikubali, na pia mbele ya Ofisi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Aidha kupitia taarifa hii, tunamuomba mhariri wa gazeti hilo, achapishe habari ya kusahihisha taarifa hizo za uzushi kwa manufaa ya wananchi na tasnia ya habari za michezo kwa ujumla.
Salum Vuai Issa
Msaidizi Katibu
TASWA-Zanzibar

0 comments:

 
Top