Watu  watano wameuwawa nchini Syria, wakati majeshi ya usalama nchini humo waliposhambualia katika miji.Makundi ya haki za binadamu nchini Syria yanasema vifo vilitokea katika mji wa kati kati wa Homs, Alhamis wakati msururu wa vifaru vilipoingia katika mji wa Qusair katika eneo hilo.Wanasema shambulizi la pili lilitokea katika mji wa kaskazini-magharibi wa Saraqeb karibu na mpaka na Uturuki. Wanaharakati hao wanasema majeshi ya usalama yalivamia nyumba kadhaa na kuwakamata watu wasiopungua 70.
Taarifa zaidi juu ya tukio hilo zimekuwa vigumu kuzipata kwa sababu serikali inawaruhusu waandishi wa habari wachache wa kigeni kuingia nchini humo na wanawadhibiti mienendo yao.
Watu wasiopungua 12 waliuwawa Jumatano katika ukandamizaji wa serikali dhidi ya wapinzani. Rais wa Syria Bashar al-Assad anazidi kulaaniwa na jumuiya ya kimataifa kutokana na ukandamizaji anaouwongoza dhidi ya wapinzani wanaomtaka aondoke madarakani. Jumatano Marekani ilitangaza vikwazo vipya dhidi ya Damascus, ikisema itazuia mali za benki ya Syria nchini Marekani na huduma za simu za mkononi. White House ilisema Syria itakuwa kwenye wakati mzuri bila ya bwana Assad.
Wakati huo huo naibu balozi wa Uingereza kwa Umoja wa Mataifa, Philip Parham, alisema Syria inafanya mashambulizi dhidi ya watu wake jambo ambalo ni ukatili na halikustahiki kutendeka, lakini Syria imekanusha matamshi hayo. Parham alizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya nchi nne za ulaya kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Alisema raia wasiopungua 2,000 wengi wasio na hatia wameuwawa nchini Syria na watu wapatao 3,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao,  baraza la usalama litaangalia njia zaidi za kuishinikiza Syria kama haisitishi msako wake dhidi ya waandamanaji wa upinzani.

0 comments:

 
Top