Chuo cha Dhow Countries Music Academy (DCMA) kimetunukiwa tuzo ya kimataifa ya Roskilde Festival World Music kwa mwaka 2010. Tuzo hiyo ni aina ya utambulizi unaopewa jumuiya au asasi zinazoleta maendeleo ya kimuziki kwa kutilia mkazo muziki wa asili – kwa ajili ya kuhakikisha mapokezi ya utamaduni kwa watoto na vijana katika nchi zinazoendelea. Tuzo hiyo imetolewa na shirika la kimisaada ya Kisanaa la Roskilde Festival Chairty Society kufuatia mapendekezo ya Tamasha la Roskilde, waandaji wa kongamano la World Music Expo (WOMEX) pamoja na Baraza la Ulaya la matamasha ya muziki duniani (European Forum of Worldwide Music Festivals).

Chuo cha DCMA kinatoa elimu ya muziki kwa vijana, kina mtazamo wa maendeleo ya tamaduni za kanda na kinajumuisha wigo wa ala za muziki asili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002.

Mradi wa DCMA utapokea TZS 65 kwa majukumu yake ya kustawisha na kuendeleza urithi wa muziki katika sehemu ambazo maendeleo ya utamaduni hayapewi kipaumbele kutokana na mahitaji ya msingi zaidi.

Peter Hvalkof kutoka Tamasha la Roskilde ameipongeza DCMA kwa mchango wao wa muda mrefu katika sekta ya utamaduni. “Chuo cha DCMA hakivutii tu kwa sababu ya dira yake na kiwango cha shabaha zake, ila pia ni taasisi inayoendeshwa kitaalamu na ambayo imedhahirisha thamani yake na kuweza kuleta tofauti katika sehemu yake.”
DCMA ni taasisi ya pili iliyowahi kutunukiwa tuzo hii ambapo katika mwaka wake wa kwanza (2009), mwanamuziki maarufu wa nchini Mali, Rokia Traore, ndiye aliyeshinda tuzo hiyo kwa kigezo cha kuasisi La Fondation Passarelle ambalo linachangia katika kukuza utaalamu katika muziki wa utamaduni wa nchi ya Mali.

DCMA imepata mwaliko wa kupokea rasmi tuzo hiyo nchini Denmark mwisho wa mwezi wa Oktoba 2010 katika hafla itakaoendana na kangamano la mwaka la wadau wa muziki asili duniani lijulikanalo kama WOMEX. Kongamano la WOMEX ndio mkutano kubwa kuliko yote ulimwenguni linalojumuisha ramsa ya kibiashara, maonesho, mikutano, soko la filamu pamoja na tuzo mbali mbali. Kongamano la mwaka huu litafanyika mjini Copenhagen, Denmark kuanzia tareher 27 hadi 31 Oktoba 2010.

“Tuzo hii ni faraja kubwa sana na shime kwa wafanyakazi, wanafunzi na bodi ya DCMA, iliyotambua miaka mingi ya kazi muhimu ya kujenga taasisi mpya ya kitamaduni na kielimu yenye umuhimu kwa sehemu yetu,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa DCMA Hilda Kiel. Kwa kuongezea alisema kuwa tuzo hiyo pia utambulisho kwa muziki wa Kiswahili na utamaduni wake pamoja na kutambua kazi ya kusomesha wanamuziki. “Tuzo imetolewa kutoa msukumo kwa vijana wanaotaka kujikita elimu ya muziki na matumaini yetu ni kuitumia vyema katika kuwawezesha na kuwashajihisha wanafunzi vijana kuchukua fursa zote zinazotolewa na DCMA na hatimaye kubaini uzuri na uwezekano wa kuwa na maisha kama mwanamuziki.”

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Chuo, Fedha hizo zilizopewa DCMA kama sehemu ya tuzo hiyo zitawekezwa katika harakati za kielimu kwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi, ununuzi wa ala na vifaa vya masomo, ununuzi wa vifaa vya sauti pamoja na kuendeleza miradi maalum ya muziki inayolenga watoto na vijana wa shuleni na vijijini.

DCMA ni taasisi isiyo ya kiserikali inaoendesha chuo cha muziki yenye mkazo katika kutoa mafunzo ya ala za muziki asilia, kozi za muziki na mitindo yenye athari za utamaduni wa jahazi wa Zanzibar pamoja na maeneo ya bahari hindi. Miradi ya watoto na vijana ya DCMA inajumuisha kozi maalum zinazofanyika Chuoni, katika shule tofauti na vijijini. Hadi sasa, Chuo kimeshawahi kupokea sifa mbali mbali ndani na nje ya nchi kama vile Tuzo ya Balozi wa Marekani ya Uhifadhi wa Utamaduni (2003), tuzo ya BBC World Music aliyotunzwa Mkuu wa Chuo Hilda Kiel (2007) na Tuzo ya muziki ya Zanzibar (2007)

0 comments:

 
Top