Na,Jumbe Ismailly-Itigi
WAKULIMA wa zao la tumbaku katika Halmashauri ya wilaya ya Itigi,wilayani Manyoni,Mkoani Singida wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo bei ndogo wakati wa kuuza mazao yao ikilinganishwa na gharama wanazotumia wakati wa msimu wa kilimo cha zao hilo.

Hayo yamebainishwa na diwani wa kata ya Mitundu,Andrea Madole Mkwawa wakati wakijadili changamoto za wakulima wa zao la tumbaku wanazopata wanapokwenda kuuza tumbaku yao kwenye makampuni yanayonunua zao hilo.

“Napenda nizungumzia changamoto za wakulima wangu wa zao la tumbaku wa kata zetu ikiwemo Mitundu tatizo lililoonekana ni kwamba benki ya CRDB ambaye ni mwezeshaji na kampuni wamekuwa wakipingana”alifafanua diwani huyo.

Alizidi kufafanua diwani huyo kuwa kupingana kwa makampuni hayo kunatokana na benki ya CRDB ikishatoa uwezeshaji kutokana na makisio yaliyowekwa na hivyo makampuni yanayonunua zao hilo hushindwa kununua tumbaku ya wakulima,hivyo aliishauri serikali kurudisha ushindani wa makampuni ya kuanzia mwaka ujao ili atakayekidhi mahitaji ya wakulima ndiye aruhusiwe kununua.

Kwa mujibu wa Madole endapo ushindani huo utakuwepo katika msimu wa kuuza zao hilo mwakani kutawasaidia kuuza na kununua zao hilo na kuondokana na madeni pamoja na kulaza madeni yao yanayosababishwa na kubaini hawapati chochote baada ya kuuza mazao yao kutokana na ujanja ujanja unaofanywa na baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu.

“Na hili tatizo limekuja kujitokeza la akulaza madeni limetokana na baada ya wakulima kuona hawapati angalau chochote ndiyo maana ujanja ujanja ukajitokeza,lakini kampuni ikikopesha pembejeo na kununua itamsaidia mkulima”alisisitiza diwani huyo.

Naye diwani wa kata ya Mwamagembe,tarafa ya Itigi,Yahaya Issah Masudi alizitaja changamoto zingine wa wakulima wa zao la tumbaku kuwa ni pamoja na benki ya CRDB kutokuwa tayari kuwakopesha wakulima wa zao hilo kwa madai kuwa bado wanakabiliwa na madeni makubwa.

Hata hivyo diwani huyo alisisitiza kuwa maamuzi hayo yaliyochukuliwa na benki hiyo hayatakuwa yamewatendea haki wakulima wa tumbaku kwa madai kwamba kuna wakulima waadilifu na watiifu wasiokuwa na madeni na kuna wakulima wasiokuwa waadilifu wanaolaza madeni ya benki hiyo.

“Maoni yangu mimi nilikuwa naona kwamba wale wakulima ambao siyo waadilifu ni bora wakafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili waweze kupata haki yao ya msingi kuliko kuwaadhibu wakulima watiifu na wasiokuwa na madeni yeyote yale katika benki hiyo.

Akizungumzia hoja za madiwani wa Halmashauri hiyo mpya ya Itigi,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Msafiri Athumani Msafiri alibainisha kwamba licha ya benki kuwachukulia hatua wakulima,lakini ni ukweli usiopingika kuwa kuna baadhi ya wakulima wenye matatizo na baadhi ya wanunuzi pia walio na matatizo.

“Na hasa inapotokea fedha pale zinapochukuliwa hapo ndipo urafiki unapotoweka,waheshimiwa mmelalamika hapa lakini tutakapochukua hatua za kumfilisi mtu msijitokeze kwamba sasa huyu atafilisika,mmenielewa?alihoji mkurugenzi huyo.

“Msije mkalalamika baadaye ikifika hatua mtu atakapokopa halafu akasababisha wenzake wakapata taabu kupitia chama cha ushirika hawapati huduma atafilisiwa mpaka alipe deni hilo”aliweka wazi Mkurugenzi mtendaji huyo.

0 comments:

 
Top