Na,Jumbe Ismailly-Itigi
MKUU wa wilaya ya Manyoni,Mkoani Singida amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano haitawavumilia watumishi wa serikali walio wazembe na wavivu na hivyo amewataka watumishi wa aina hiyo waanze kujiandaa kukabidhi ofisi kwa watumishi watakaoendana na kasi ya Rais,Dk.John Pombe Magufuli.

Mkuu wa wilaya huyo,Fatma Hassani Toufiq alitoa rai hiyo kwenye mkutano wa kwanza wa Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Itigi,uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano mjini hapa.

“Natoa rai kwa watumishi wa serikali ambao hasa ni wazembe na wavivu kujiandaa kwani hawatavumiliwa katika serikali itakayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dk.John Pombe Magufuli”alisisitiza mkuu wa wilaya huyo.

Kwa mujibu wa Toufiq lugha za hiyo ni changamoto, tunashughulikia au mchakato unaendelea,havitavumiliwa katika serikali ya awamu ya tano na kuongeza kwamba muda wa kuwalea watu wanaolipwa mishahara lakini hawafanyikazi wanazotakiwa kufanya au waliogeuza ofisi za umma kuwa ni mahali pa kuchuma bila kufanyakazi.

Aidha Toufiq aliweka bayana kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika okt,mwaka huu,wananchi walilalamikia kero mbalimbali zikiwemo za upotevu wa mapato,kushindwa kukusanya ushuru na tozo mbalimbali,matumizi mabaya ya fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya kiwango,wizi,uzembe,migogoro ya ardhi na kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Supeet Roine Mseya akiongea na madiwani pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Itigi aliweka bayana kwamba wananchi wa jimbo la Manyoni magharibi walianza kudai Halmashauri hiyo tangu mwaka 1988.

“Lakini tu niseme Halmashauri ya wilaya ya Itigi wananchi wameanza kuidai tangu mwaka 1988,lakini nilipofika mwaka 2013 kati ya mambo ambayo nilimuomba mungu aniwezeshe ni kuhakikisha hoja za wananchi wa itigi zinatimia”alisema Mseya.

Awali katibu tawala wa wilaya ya Manyoni,Cosmas P. Sikali akifungua mkutano wa uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo alisema wanapozungumza suala la serikali za mitaa ina maana ni serikali ambayo ipo karibu sana na wananchi.

Aidha Sikali alibainisha kuwa serikali za mitaa zitawezesha wananchi kutambua ni kiasi gani wanashirikishwa katika mambo mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maendeleo endelevu sambamba na kuwafanya wawe karibu sana na wawakilishi wao ambao ni madiwani.

0 comments:

 
Top