Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi leo amekabidhi vifaa vya michezo kwa Timu 60 za Mpira wa soka zilizomo ndani ya Jimbo hilo ili kusaidia nguvu na chachu ya kuimarisha Michezo katika Jimbo la Kitope.

Vifaa hivyo ambavyo ni seti za Jezi na Mipira vyenye Thamani ya shilingi Milioni Nane, Laki Nne na Hamsini Elfu { 8,450,000/- } vimekabidhiwa kwa timu hizo hapo Kipandoni Wadi ya Upenja Wilaya ya Kaskazini “B”.

Balozi Seif akiambatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi pamoja na baadhi ya Viongozi wa Wadi ya Upenja na Jimbo la Kitope akikabidhi Seti za Jezi na Mipira kwa Timu za Jimbo hilo zinazoshiriki Ligi ya Kanda ya Unguja,Daraja la Pili na daraja la Tatu.

Na pia akakabidhi mipira kwa 36 ya Mitaani pamoja na timu mbili za watoto wadogo wa Kijiji cha Kipandoni na kuahidi kuonyesha nia ya kusaidia kuwatengenezea Kiwanja watakachokichaguwa ili kiwe na hadhi ya michezo ya Kitaifa ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.

Akizungumza na Wanamichezo hao Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi aliwataka Vijana hao kujiepusha na makundi ya baadhi ya watu wanaojaribu kuwashawishi wajiingize katika mambo yaliyo nje ya Sekta ya Michezo.

Balozi Seif alisema ni vyema kwa vijana hao wakaendelea kuwaamini Viongozi waliokubali kuwatumikia katika mambo na harakati zao za kila siku hasa zile za michezo ambazo kwa sasa husaidia kutoa ajira.

Aliwataka wanamichezo hao kupitia Viongozi wao waangalie utaratibu wa kutafuta kiwanja kitakachowekewa miundo mbinu ambayo baadaye kitakidhi mahitaji ya kuchezewa Ligi yenye hadhi ya Kitaifa.

Mapema Mke wa Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi alisema katika kuunga mkono juhudi za wanamichezo hao alisema ni vyema kwa wanasoka hao wanzishe utaratibu wa kuanza kuchangia hata kwa kiwango kidogo ili kuwapa nguvu Viongozi na wafadhili wanaoonyesha nia ya kuwasaidia.

Mama Asha alisema Viongozi wa Jimbo hilo watashawishika na kuongeza nguvu zao kwa Timu ambazo tayari zimeshajikubalisha kujisaidia zenyewe zikisubiri nguvu za ziada.

Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar Wilaya ya Kaskazini “ B” Tongoa Moh’d Hassan alisema Wilaya hiyo bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa Kiwanja cha soka chenye hadhi inayokubalika kwa michezo mikubwa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top