Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba karne iliyopo hivi sasa ya 21 ambayo imebeba Sayansi na Teknolojia ulimwenguni haistahiki watoto wa kizazi chake kuendelea kupata elimu katika mazingira duni.
Alisema juhudi za ziada kwa wazazi, wazee pamoja na Viongozi kwa kushirikiana na Kamati za Maskuli zinapaswa kuchukuliwa ili kuona watoto wote Nchini wanaendelea kujengewa mazingira yanayokwenda na karne hiyo.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza hayo kwa nyakati tofauti wakati akikabidhi vikalio 75 kwa ajili ya Skuli za Upenja na Pwani Kiwengwa akitekeleza ahadi alizotoa kwa Walimu, Wanafunzi na Kamati za Skuli hizo.
Vikalio 45 viligaiwa kwa Skuli ya Msingi na Sekondari ya Upenja wakati vyengine 30 vikakabidhiwa kukamilisha Madarasa yote ya Skuli ya Kiwengwa yakiwa na vikalio kamili vyote vikiwa na thamani ya Shilingi Milioni Kumi na Mbili na Laki Tano { 12,500,000 }.
Balozi Seif alisema ipo haja kwa viongozi wa Majimbo kuongeza nguvu zao katika kusaidia huduma za Elimu ili kuiunga Mkono Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ambayo kwa sasa ina majukumu mengi ya kukamilisha majengo yaliyoanzishwa kwa michango na nguvu za Wananchi wenyewe.
Alitoa mfano wa jukumu kubwa linaloikabili Wizara ya elimu ya kuzipatia vikalio Skuli zote za Unguja na Pemba ambapo bado kwa sasa upo upungufu mkubwa wa vikalio vipatavyo 25 elfu Zanzibar nzima.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali haijawa na nguvu kamili ya kuzipatia skuli zote za Zanzibar Vikalio kwani Wizara hiyo hivi sasa ina mambo mengi ya kufanya likiwemo changamoto la uwezekaji wa majengo yaliyoanzishwa na wananchi katika maeneo yao.
Alieleza kwamba Taifa linahitaji kuwa na viongozi wengi wenye sifa zinazokubalika Kitaaluma, lakini hilo halitapatikana endapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa na kuanzishwa na Viongozi katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi na Walimu katika skuli mbali mbali hapa Nchini.
“ Mimi kama Mbunge wa Jimbo hili sitasita kuendelea kusaidia maendeleo ya Kielimu hata nje ya Jimbo langu kutokana na wadhifa niliyokuwa nao hivi sasa wa Umakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar “. Alisema Balozi Seif.
Aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi kubwa zinazochukuliwa na Wananchi wa Jimbo la Kitope kwa muamko wao wa kuanzishwa majengo mapya ya Madarasa kwenye skuli mbali mbali za Jimbo hilo
Balozi Seif alisema katika kuunga mkono juhudi za Wananchi pamoja na walimu atajitahidi ili kuona nyumba za Walimu zilizojengwa katika skuli za Upenja na Kiwengwa zinakamilika ili kuwaondoshea usumbufu walimu wa skuli hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alilipongeza Wazo la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar la kuitaka Jamii inapojenga majengo mapya ya madarasa katika maeneo yao yakaenda sambamba na ujenzi wa nyumba za Walimu.
Balozi Seif alifahamisha kwamba hatua hiyo muhimu kwa kiasi kikubwa itawapa fursa na wasaa mpana walimu kuweza kuwapatia taaluma wanafunzi wao kwa nyakati zote ukiwemo ule muda wa ziada.
Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Sekondari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Bibi Asya Iddi Issa alisema msaada huo wa Vikalio kwa Skuli za Upenja na Kiwengwa uliotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi umeipa msukumo Wizara hiyo katika kupunguza uhaba wa vikalio kwa skuli mbali mbali hapa Nchini.
Bibi Asya ameitahadharisha Jamii kujiepusha na wizi wa vifaa vya Maskuli ambao hurejesha nyuma juhudi za wahisani pamoja na viongozi wanaoamua kusaidia vifaa hivyo kwa lengo la kupunguza changamoto zinazojitokeza ndani ya sekta ya Elimu.
Alisema upo ushahidi na baadhi ya matukio yaliyojichomoza kwa baadhi ya watu kuiba vifaa hivyo hasa vikalio kwa kutengeneza vifaa vyengine na baadaye kuuza jambo ambalo si utu wala uungwana kuendeleza tabia hiyo mbaya.
Wakitoa shukrani kwa niaba ya wazazi, Walimu na Wanafunzi wa Skuli za Upenja na Kiwengwa Walimu Wakuu wa Skuli hizo Mwalimu Jaffar Ali Haji wa Upenja na Mwalimu Ali Mtumwa Ussi wa Kiwengwa walielezea faraja yao kutokana na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Mbunge wa Jimbo lao Balozi Seif Ali Iddi.
Maalim Jaffar Ali aliiomba Serikali ifanye utaratibu wa kuushawishi Uongozi wa Benki ya Wananchi wa Zanzibar { PBZ } kufungua Tawi la Benki hiyo ndani ya Mkoa wa Kaskazini ili kuwapunguzia usumbufu wa kukatisha vipindi Walimu wao wakati Mwalimu Ali Mtumwa wa Kiwenga akaeleza kwamba Skuli hiyo imejipanga kutoa elimu ya maandalizi katika kiwango kitakachokuwa mfano ndani ya Mkoa huo.
Katika kuchangia juhudi za Walimu, Kamati ya Skuli na Wanafunzi wa Skuli ya Kiwengwa Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi alikabidhi mchango wa shilingi Milioni moja { 1,000,000/- } kusaidia uendelezaji wa Nyumba Walimu wa skuli hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment