Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Jamuhuri ya Ireland kuitumia fursa ya uwekezaji iliyopo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi na maendeleo.

Alisema uwekezaji wa washirika hao wa maendeleo nchini Tanzania utaongeza nguvu katika kuimairisha uhusiano wa Kidiplomasia uliopo kati ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Ireland.

Akizungumza na Ujumbe wa Jamuhuri ya Ireland ukiongozwa na Waziri wa Nchi Maendeleo ya Biashara na Ushirikaino wa Ireland Bwana Sean Sherlock hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Zanzibar na Tanzania bado zina mazingira mazuri na rasilmali zinazoweza kutumika katika uwekezaji.

Balozi Seif aliwahakikishia wawekezaji wa Ireland kwamba licha ya kwamba Taifa la Tanzania linakabiliwa na kura ya Maoni pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka huu lakini litaendelea kubakia katika hali ya amani na utulivu.

“ Tunawatoa hofu wa Irish watakaoamua kuja kuwekeza miradi yao ya kibiashara kwa kusaidia uchumi ya Nchi wasiwe na wasi wasi wowote kwani Tanzania itaendelea kubakia kuwa kisiwa cha amani Duniani “. Alisema Balozi Seif.

Naye Waziri wa Nchi Maendeleo ya Biashara na Ushirikiano wa Ireland Bwana Sean Sherlock alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba uhusiano kati ya Ireland na Tanzania utaendelea kuimarishwa Kwa ustawi wa Wananchi wa pande zote mbili.

Bwana Sean Sherlock`alisema uhusiano huo utaelekezwa zaidi katika kuona wataalamu wa sekta mbali mbali za Maendeleo wa Ireland hasa katika sekta ya Kilimo na utalii wanaongeza nguvu zao za kitaalamu kwa kusaidia wataalamu wazalendo.

Waziri wa Nchi Maendeleo ya Biashara na Ushirikaino wa Ireland Bwana Sean Sherlock alisisitiza kwamba Nchi yake itajitahidi kuunga mkono juhudi za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kusaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi zinazoonekana kuiikumba Dunia hivi sasa.

Mapema Waziri wa Kilimo na Mali Asili Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya aliueleza Ujumbe huo wa Ireland kwamba uimarishaji wa miundo mbinu katika Sekta ya Kilimo ni jambo la msingi lililopewa kipaumbele na Wizara hiyo.

Dr. Sira alisema hatua hiyo ya Serikali kupitia Wizara husika ya Kilimo imekuja kufuatia Wananchi walio wengi ndani ya Visiwa vya Zanzibar ambao wanafikia zaidi ya asilimia 80% wanaendesha maisha yao kwa kutegemea sekta mama ya kilimo.

Alifahamisha kwamba Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar inaendelea ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi ikitumia wataalamu wake kwa kushirikiana na washirika wa Maendeleo ndani na nje ya Nchi.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar Bibi Amina Khamis alisema Dira ya Maendeleo ya Zanzibar imeundwa maalum na Serikali kuu kwa lengo la kusaidia mipango ya Maendeleo katika kuimarisha Kiuchumi.

Bibi Amina alisema Mpango wa kupunguza umaskini Zanzibar MKUZA umetoa fursa pana zaidi katika sekta za Kilimo na Utalii ambazo zimeonyesha muelekeo wa mzuri wa kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira unaowakumba zaidi Vijana wanaomaliza masomo yao ya sekondari.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top