Timu ya Soka ya West Star ya Shehia ya Kijiji cha Pangeni ndani ya Jimbo la Kitope Wilaya ya Kaskazini “B” imeibuka mshindi dhidi ya wapinzani wake Timu ya Soka ya Spider ya Kijiji hicho kwa kuilaza magoli 4-2 kwenye pambano la Fainali ya Kombe la Mbuzi lililopigwa katika Uwanja wa michezo wa Kijiji hicho.

Mashindano ya Kombe hilo lililoandaliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Vugu vugu la kufufua michezo ya ndani ambae pia ni Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi lilijumuisha takriban Timu Nane za Soka za Shehia ya Pangeni yalianza rasmi Tarehe 28 Agosti 2013 kwa mfumo wa ligi katika makundi mawili.

Mabingwa hao West Star waliovalia jezi za mistari rangi nyeupe kwa bahari walijipatia ushindi huo kwa njia ya penalti baada ya timu hizo kwenda sare bila ya kufungana hadi mwisho wa mchezo huo ambapo mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi.

Timu hizo licha ya kutofungana katika dakika 90 za mchezo huo lakini zilikuwa zikishambuliana kwa zamu wakionekana Spider kuutawala zaidi mchezo huo wa fainal katika kipindi cha kwanza wakati muda mwingi wa kipindi cha piki ukawapa zamu ya West Star kufanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Spider.

Akizungumza mara baada ya kupatikana mshindi wa fainali hiyo Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema lengo la kuandaliwa kwa mashindano hayo ni kuwajenga zaidi vijana kimichezo ili kuepukana na vigenge vinavyochangia upotoshaji wa maadili.

Balozi Seif alisema Uongozi wa Jimbo hilo utaendelea kuunga mkono michezo ya vijana ndani ya jimbo hilo ili kuwajengea nguvu na uwezo wa kushiriki vizuri katika mashindano ya Kitaifa hapa nchini.

Alielezea kufurahishwa kwake na vugu vugu la michezo linaloendelea kuonyeshwa na vijana sehemu mbali mbali nchini hali inatotoa fursa ya kuanza harakati za kuvipata vipaji walivyonavyo baadhi ya Vijana katika maeneo tofauti.

“ Kiwango cha mchezo mliouonyesha katika pambano lenu hili la fainali limewafanya hata baadhi ya wasaidizi wangu niliofuatana nao kushuhudia pambambano hili kushabikia timu hizi “. Alifafanua Balozi Seif.

Katika Fainali hiyo ya Kombe la Mbuzi Mbunge huyo wa Kitope alikabidhi Jezi seti moja, Mbuzi Wawili, Mpira Mmoja na Fedha Taslimu 150,000/- kwa mshindi wa kwanza West Star.

Balozi Seif alimkabidhi Mshindi wa Pili Spider Jezi Seti moja, Mpira Mmoja, na shilingi Laki 150,000/- wakati mshindi watatu Timu ya Soka ya Sabwengo ikapata zawadi ya jezi seti moja na Mpira Mmoja.

Tumu nyengine Sita zilizoshiriki ligi hiyo ya Kombe la Mbuzi la Shehia ya Pangeni walikabidhiwa zawadi ya Mpira mmoja, pamoja na shilingi 50,000/- kwa kila Mchezji bora,muamuzi, Bora, Mfungaji Bora, Kipa Bora, Timu Bora na Mchezaji Mdogo kuliko wote katika mashindano hayo.

Timu zilizoshiriki katika mashindano hayo ya kombe la Mbuzi la Shehia ya Pangeni yaliyogharimu zaidi ya Shilingi Milioni 1,800,000/- zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif ni pamoja na Timu za Jiko la Shamba, White Star, New Kid Star, New Small Tiger, Sabwengo, Maumivu pamoja na Ukombozi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top